Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato(ATAPE), kimekusudia kuwekeza katika ujenzi wa mradi wa maji kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi  na ujenzi wa hosteli ili kutoa huduma za malazi katika Mkoa wa Simiyu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freddie Manento alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kusekwa Memorial Mjini Bariadi, ambako umefanyika Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho kwa takribani siku saba ambao umeanza Aprili 16 na utahitimishwa Aprili 21, 2019.

Amesema kuwa ATAPE imedhamiria kuwekeza kwenye miradi itakayokuwa na tija kwa Watanzania wote kwa ujumla huku akieleza kuwa timu ya wataalam wa uwekezaji wa chama hicho inaendelea kufanya utafiti, ili kubaini eneo litakalofaa kuchimba kisima cha maji na kujenga hosteli mkoani Simiyu.

“Tumedhamiria kuacha alama katika Mkoa wa Simiyu kupitia mkutano wetu wa 20 wa ATAPE, tumepewa fursa ya kiwanja kwa ajili ya kujenga hosteli katika kukabiliana na changamoto ya malazi, lakini pia wataalam wetu wanaendelea na utafiti kubaini mahali tutakapochimba kisima kwa ajili ya huduma ya maji kwa Wanasimiyu” amesema Manento

Pamoja na miradi hiyo inayotarajiwa kutekelezwa mkoani Simiyu, Manento amesema ATAPE imewekeza katika kilimo kwenye mashamba ya miti, miwa, mikorosho, miti ya miparachichi ambayo kwa ujumla yana ukubwa wa ekari 10,000 na ekari zaidi 3500 ambazo zinatarajiwa kufanyiwa uwekezaji mwingine.

Amesema  hadi sasa ni takribani shilingi bilioni 1.039 imewekezwa katika miradi hiyo ambayo pia imechangia kutoa ajira za kudumu na za msimu kwa Watanzania walio katika maeneo yenye miradi hiyo, huku akibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo hayo ATAPE imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii husika.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa ATAPE ametoa wito kwa wananchi mkoani Simiyu hususani Bariadi kutumia mkutano huo kama fursa kiuchumi kupitia biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri wa kuwatoa na kuwapeleka wajumbe katika eneo la mkutano.

Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu wamesema Mkutano wa ATAPE umekuwa fursa kwao kwa kuwa utawasaidia kujiingizia kipato na kupata ujuzi mpya kupitia huduma na bidhaa zitakazouzwa kwenye mkutano huo.

Mabomu yalipuka ndani ya makanisa matatu Sri Lanka Jumapili ya Pasaka
Picha: Mabegi, magunia ya pesa yaliyokutwa nyumbani kwa al-Bashir yawekwa wazi