Ratiba ya safari za ndege mpya za Serikali aina ya Bombardier Q400 zilizozinduliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli imeanza kutajwa huku upungufu  wa ndege zinazofanya safari ndani ya nchi ukiwasumbua wasafiri.

Baadhi ya wasafiri waliokuwa wanatumia ndege za Fastjet wameonekana kukwama katika viwanja vya ndege vya Songwe na Mwanza baada ya kampuni hiyo yenye sifa ya kuwa na viwango nafuu vya nauli nchini kupunguza idadi ya ndege zake kutoka tatu hadi moja.

Kutokana na upungufu wa usafiri huo ndani ya nchi, baadhi ya abiria waliokumbwa na tatizo hilo katika viwanja hivyo vya ndege waliiomba Serikali kuruhusu ndege hizo mpya zilizokodishwa kwa kampuni ya ndege ya ATCL kuanza kutoa huduma mara moja ili kuwaokoa wananachi na mkwamo huo wa usafiri.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotaka kufahamu ratiba ya kuanza safari kwa ndege hizo, jana maofisa wa ATCL walisema kuwa ndege hizo zinaweza kuanza safari zake mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo.

Maofisa hao walieleza kuwa tayari taratibu za kisheria kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) umekamilika na kwamba ndege hizo zinazosifiwa kwa kutumia gharama ndogo za uendeshaji wake ziko tayari kutoa huduma.

Ndege hizo za kisasa zina uwezo wa kusafiri kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kilimanjaro, Kigoma bila ya kuongeza mafuta ya ziada ya yale iliyojaza Dar es Salaam. Pia, imetajwa kuwa na uwezo wa kutua katika Mikoa  yenye viwanja vya changalawe na vidogo visivyofikiwa na ndege kubwa aina ya Boeing.  Hivyo, zinategemewa kuwa mkombozi mkubwa kwa watumiaji wa usafiri wa anga nchini.

Video: Rais wa Congo, Joseph Kabila kuweka jiwe la msingi jengo la TPA leo
Mitandao yamtumbulisha Polisi aliyeomba rushwa kwa mtalii Zanzibar