Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imewasafirisha abiria 200 kwenda chini India, waliokuwa wamekwama nchini kutokana na marufuku ya kufanya safari za anga za nje ya nchi, iliyowekwa Machi 25, 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kuwa wakati ndege hiyo inarejea, itawarudisha abiria 180 wa Tanzania waliokuwa wamekwama nchini India.

Alisema kuwa kutokana na marufuku ya safari za anga kutoka na kuingia nchini kama hatua ya kupambana na mlipuko wa virusi vipya vya corona (covid-19), abiria wengi waliokuwa wanatarajia kusafiri kati ya India na Tanzania walikwama.

“Tunaishukuru Serikali ya India kupitia ubalozi wake kwa ushirikiano wao hasa katika kipindi hiki ambacho wamesitisha usafiri wa anga ndani ya nchi yao,” alisema Mhandisi Matindi.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha corona, ATCL iliendelea kutoa huduma ya usafiri ndani ya nchi kupitia viwanja 11, huku ikichukua tahadhari zote dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Sanjiv Kohli, alisema kuwa wamefurahi kuwa wananchi wake 200 wanaruhusiwa kurejea nyumbani.

“Watu hao wamerejea nyumbani kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sababu za kupata matibabu na kufanya biashara, na baadhi yao wanatarajia kurejea Tanzania baada ya safari hiyo,” alisema Balozi Kohli.

Alisema kuwa India itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho Dunia inapambana na mlipuko wa virusi vya corona.

Rwanda yaripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona

Polisi wanasa pikipiki 825 zilizoibiwa, waanika mbinu zilizotumiwa na wezi

Kazi za waandishi wa habari kufanywa na roboti, Microsoft yawafuta kazi waandishi wake
Rwanda yaripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona