Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) hatimaye imeweka wazi tarehe rasmi ya kuanza kurusha ndege zake tatu ikiwa ni pamoja na ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400 zitakazoanza kufanya safari zake kwa awamu.

Kaimu Afisa Mahusiano ya Umma wa shirika hilo, Lilly Fungamtama aliwaambia waandishi wa habari kuwa wataanza kurusha ndege hizo Oktoba 15 mwaka huu wakianza na safari kati ya Dar es Salaam na Mwanza, Dar es Salaam na Arusha na safari nyingine itakuwa kati ya Dar es Saalam na Mbeya.

Akizungumzia nauli ya ndege hizo zinazosubiriwa kwa hamu, Fungamtama alisema kuwa kwa safari moja abiria atatakiwa kulipia shilingi 160,000.

“Bombardier mbili zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ile nyingine CRJ 100s inaweza kubeba abiria 50,” alisema.

Aliongeza kuwa hadi kukamilika kwa awamu zote, ndege hizo zitafanya safari zake katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Kilimanjaro, Kagera, Dodoma na Katavi huku safari za kimataifa zikitarajiwa kuwa za Nairobi, Entebbe na Comoro.

Alisema kuwa ndege hizo zimekamilisha taratibu chini ya Mamla ya anga nchini pamoja na kuwapatia mafunzo maalum marubani wake, tayari kwa kuanza kutoa huduma.

Kuanza rasmi kwa safari za anga kwa ndege hizo kunatarajiwa kuleta ushindani mkubwa kati ya makampuni ya ATCL, Fastjet na Precision Air hivyo kuwapa unafuu zaidi Watanzania wanaotumia usafiri huo.

China yajadili kumng’oa Kiongozi wa Korea Kaskazini na jeshi lake
Video: Kiwanda cha viroba chapigwa faini Shil. mil. 25, chapewa siku 7