Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kuwa jeshi hilo limshikilia Joyce Matingo (26) mkazi wa Unyamwanga, Wilaya ya Rungwe humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda Kuzaga ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ameeleza kuwa tukio hilo ni la Januari 8 mwaka huu saa 12:00 jioni.

Amesema, siku hiyo mtuhumiwa alimfunga kamba mikono na miguu mtoto huyo, Emily mwenye umri wa miaka tisa na kuanza kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake.

Aidha ameeleza kuwa mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Unyamwanga wilayani Rungwe, alituhumiwa kuiba Sh 16,000 awamu ya kwanza na Sh 40,000 awamu ya pili zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya nyumba wanayoishi.

Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kutoa adhabu zilizopitiliza na kusababisha madhara.

Kesi ya Mkurugenzi wa Jatu bado mbichi
Juma Mgunda: Wamesema wao, sijalalamika