Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Senegal, Macky Sall ameomba Viongozi wa Afrika kupewa kiti cha uwakilishi ndani ya kundi la G20 ili Waafrika washiriki katika maamuzi yao na kusema kupanda kwa gharama za maisha, kuongezeka kwa joto, vita vya Ukraine na janga la Uviko-19, kumesababisha hali kuwa mbaya ulimwenguni.

Katika mkutano huo mkuu wa kwanza kufanyika tangu mwaka 2020, Sall pia alisisitiza wito wake wa uwakilishi bora wa Afrika katika jukwaa la dunia, kwa kusemaa angependa kukumbusha ombi hilo la AU kuwa ndani ya G20, ili Afrika ishiriki kuamua hatma yao kwani uamuzi wa pekee unaofanywa na kundi hilo bila uwakilishi wa AU unawaathiri Waafrika 1,400,000,000.

Sall, alikuwa akizungumza katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na amesisitiza kuwa, “Suala la mapigano si la Afrika pekee bali ni tishio la kimataifa lililo chini ya usimamizi wa Baraza la Usalama la (UN), ambaye ni mdhamini wa utaratibu wa pamoja wa usalama, chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Senegal, Macky Sall. Picha na BBC.

Rais huyo wa Senegal, pia aliomba kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa kwa nchi ya Zimbabwe na kusisitiza kuwa Afrika haitaki kuwa chimbuko la Vita Baridi vipya, huku akigusia shinikizo linaloongezeka kwa viongozi wa bara hilo kuchagua kukaa upande wanaoona ni salama kwao katika vita vya Ukraine.

Nchi nyingi za Kiafrika, zinategemea uagizaji wa nafaka kutoka Urusi na Ukraine ambapo sasa kuna uhaba wa soko na tayari Waziri wa mambo ya nje wa Urusi amezilaumu nchi za Magharibi kwa kupandisha bei ya vyakula huku Viongozi wa nchi za Magharibi wakiishutumu Kremlin kwa kutumia chakula kama silaha na kuendesha vita vya ushindi kwa mtindo wa kifalme.

Baadhi ya waangalizi wamezitaja juhudi za Urusi na Marekani kuwa kampeni zenye nguvu zaidi za ushawishi tangu Vita Baridi wakati bara hilo lilipokumbwa na vita vya wakala huku Marekani na Umoja wa Kisovieti zikiwania ushawishi.

Rais wa Senegal, Macky Sall. Picha na kurasa ya Ubalozi wa Senegal.

Hata hivyo, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa, Naledi Pandor alisema upo umuhimu wa kutafuta mwisho wa vita vya Ukraine wazo ambalo lilitolewa hivi karibuni na Rais wa Afrika ya Kusini Cyrill Ramaphosa ambaye anatarajia kushiriki mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki ijayo.

Ally Mayay: Nilishtushwa na uteuzi, nimesikia maagizo ya waziri
Ally Mayay apongeza kambi Serengeti Girls