Jeshi la Polisi mkoani Tanga limefanikiwa kukamata majambazi wawili waliohusika na matukio mbali mbali ya uhalifu mkoani humo.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, RPC Benedict Wakulyamba wakati akizungumza na dar24.com ambapo ametoa taarifa hizo za kukamata majambazi wawili waliokiri kuhusika moja kwa moja katika uvamizi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) kilichopo wilaya ya Lushoto mkoani humo hivi karibuni na kumuua mlinzi katika chuo hicho.

Kamanda huyo amesema kati ya vitu vilivyokamatwa pamoja na majambazi hao ni bunduki 9 ambapo mojawapo ni ile iliyoporwa kwa mlinzi wa chuo cha SEKOMU. Hata hivyo, amesema jeshi la Polisi Tanga linaendelea na upelelezi likishirikiana na wananchi kupitia sera ya Polisi jamii kukamata wahalifu kokote walipo.

Akizungumzia hali ya usalama mkoani humo amesema hali kwa sasa ni shwari kabisa na amani, hata wanachuo sasa wana amani, hivyo amewataka wananchi wasiwe na hofu yoyote waendelee na shughuli zao kwani Jeshi la Polisi lipo imara na tayari kupambana na uhalifu wa aina zote.

Serikali Kupunguza gharama za mawasiliano
Tanzia: Mwanamuziki nguli Achieng Abura afariki dunia