Timu ya taifa ya Austria imekata tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Ulaya za mwaka 2016 baada ya kuikandamiza timu ya taifa ya Sweden mabao manne kwa moja usiku wa kuamkia hii leo.

Austria wamepata ushindi huo wakiwa ugenini, hali ambayo ilikua haitarajiwi na mashabiki wengi ulimwenguni kote kutokana na muonekano wa kikosi cha timu ya taifa ya Sweden ambacho kimesheheni wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kisoka.

Mabao ya Austria yalipachikwa kimiani na beki wa pembeni David Alaba, Marc Janko pamoja na Martin Harnik aliyefunga mabao mawili huku bao la wenyeji likifungwa na Zlatan Ibrahimovic katika dakika ya 90.

Ushindi huo unaiwezesha Austria kufikisha point 22 katika msimamo wa kundi la saba, ikifuatiwa na timu ya taifa ya Urusi yenye point 14 na Sweden inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na point 12.

Timu nyingine zilizopo kwenye kundi hilo ni Montenegro wenye point 11, wakifuatiwa na Liechtenstein wenye point tano na Moldova wanaburuza mkia kwa kuwa na point 2.

Austria wanajiunga na timu za England, Jamuhuri ya Czech, Iceland pamoja na wenyeji Ufaransa ambazo zimeshatinga kwenye fainali za mwaka 2016 ambazo zitaanza kuunguruma June 10 – July 10.

Timu 24 zinatarajiwa kupambana kati michuano hiyo ambayo imekua na msisimko mkubwa kutokana na ushindani wa kisoka uliopo baina ya timu za mataifa ya barani Ulaya.

Rooney Ampiku Sir Bobby Charlton England
Kubenea: Dk Slaa Anajua Hoja Ya Richmond Na Lowassa Haipo, Kuna Ripoti Mbili Tofauti