Chama cha soka nchini Urusi (RFU), kimetangaza adhabu kwa meneja wa klabu ya Zenit St Petersburg, Andre Villas-Boas kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha dhidi ya muamuzi namba nne wakati wa mchezo wa ligi ya nchini humo uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

RFU wametangaza adhabu hiyo kwa Andre Villas-Boas kupitia kamati yake ya nidhamu ambayo ilifikishiwa kesi hiyo mara baada ya mchezo wa ligi ambapo Zenit St Petersburg walikubali kupoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Krylya Sovietov.

Villas-Boas alikua akituhumiwa kumsukuma muamuzi namba nne wa mchezo huo, na kamati ya nidhamu ya RFU ilipojiridhisha kwa ushahidi wa picha za televisheni ilibaini ukweli wa jambo hilo na kufikia maamuzi ya kumfungia kukaa kwenye benchi la ufundi kwa michezo sita inayofuata.

Baada ya kitendo cha kumsukuma muamuzi namba nne, meneja huyo ambaye aliwahi kuzinoa klabu za Chelsea pamoja na Tottenham Hotspur zote za nchini England, aliadhibiwa kwa kutakiwa kuondoka kwenye benchi la ufundi la Zenit na kuamuriwa kwenda kukaa jukwaani.

Matokeo ya kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Krylya Sovietov, kunaifanywa klabu ya Zenit kuwa katika mazingira magumu ya kutetea taji la nchini Urusi ambapo kwa sasa wanaendelea kukamata namba tatu kwenye msimamo wa ligi huku michezo saba ikisalia kabla ya msimu kufikia kikomo.

Lowassa Kuibua Mapya Urais
Mkwasa: Nipo Tayari Kwa Mtanange Wa Kesho