Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa siku 30 kwa watendaji wa Sekta ya Maji Handeni kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana na kuboresha uendeshaji wananchi wapate Maji.

Waziri Aweso ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea vyanzo na miradi ya maji wilayani Handeni.

Aidha, Waziri Aweso amemuagiza Mkurugenzi wa idara ya usambazaji maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Maji CPA. Joyce Msiru na timu ya wataalamu toka wizarani kubaki Handeni kuhakikisha wanakuja na mkakati mahususi wa kutatua kero ya upatikanaji wa huduma ya Maji Handeni Mjini ikiwa vyanzo vya Maji vipo.

Wakati huohuo Waziri Aweso amefanya mabadiliko ya kiutendaji na kuahidi kuleta nguvu mpya itakayoboresha eneo la uendeshaji na usimamizi ili kuleta mabadiliko Mji wa Handeni na viunga vyake.

Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 21 katika Mkoa wa Tanga ili kutekeleza miradi ya maji vijijini ikiwemo wilaya ya Handeni.

Katika hatua nyingine Wizara ya Maji ipo katika hatua za mwisho katika kukamilisha zabuni ya utekelezaji wa miradi ya maji kwenye miji 28 nchini ambapo pia utekelezaji wa mradi wa HTM utakwenda kukamilika na kumaliza kabisa changamoto ya maji wilayani Handeni iliodumu kwa kipindi kirefu.

Tarehe ya Uchaguzi yatangazwa Jimbo la Ushetu
Madereva wa Serikali watakiwa kufuata sheria