Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemuagiza mhandisi wa maji mkoani Kagera kumsimamisha kazi mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wilayani Kyerwa kutokana na kutokuwa na uwezo pamoja na vigezo.

Ametoa agizo hilo wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika wilaya za Karagwe na Kyerwa ambapo imeonekana miradi mingi ya maji katika wilaya hizo haijakamilika ambapo ni kutokana na wakandarasi wanaopewa kujenga miradi hiyo kutokuwa na uwezo.

Aweso ameonyesha kusikitishwa kwa kutokamilika kwa mradi ambao unathamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 wa Kaisio Isingilo uliokwama kwa zaidi ya miaka 5 ukiwa utekelezaji wake ni 50% na kumuagiza mhandisi mkoa kumuondoa mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

”Nikuulize mhandisi wa maji mkoa, huyu mkandarasi ana uwezo ama hana?basi kama hana nakuagiza kamuondoa mara moja, na mtafute mwingine haraka mwenye uwezo wa kifedha atekeleze haraka mradi huu, na sisi tutamlipa,”amesema Aweso

Aidha, amewataka wahandisi wa maji nchi nzima kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na kuwasimamia makandarasi wanaotekeleza miradi ya maji kote nchini kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kyerwa, Innocent Bilakwate amemuomba Naibu waziri kuwasaidia wananachi wa jimbo hilo kusimamia miradi yote ya maji ili kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi hao.

Hata hivyo, naibu waziri huyo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kagera ikiwa na lengo la kuangalia na kukagua miradi ya maji katika mkoa huo

Kwandikwa ahimiza ushirikiano kutatua changamoto za elimu
Wazee 25499 kutibiwa bure wilayani Magu