Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwa na mkakati wa kutumia vifaa vya kisasa katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Waziri Aweso amesema hayo wakati akipokea taarifa ya RUWASA kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji ya vijijini tangu ilipoanza kazi Julai 2019, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Maji Jijini Dodoma.

Waziri Aweso amesema ni muhimu RUWASA ikawa na vifaa vyake vya kisasa ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maji, iweze kumaliza kwa wakati sambamba na kupunguza gharama kwa kuwatumia wakandarasi.

“Tunachohitaji ni kuona miradi inakamilika kwa wakati, Serikali ipo tayari kutoa fedha za kuhakikisha RUWASA inakuwa na vifaa vya kisasa kabisa,” Waziri Aweso amesema.

Aidha, amesisitiza wataalamu kwenye Sekta ya Maji kuhakikisha wanatumia vyema taaluma zao ili falsafa ya kumtua Mama ndoo kichwani sambamba na kaulimbiu ya RUWASA ya Maji bombani itimie kikamilifu.

Wakati wa tukio hilo la upokeaji wa taarifa, Waziri Aweso amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo, kufanya tathmini ya Wahandisi wa maji wa RUWASA ili kujiridhisha na weledi na utayari wao wa kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi.

“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kumtua mwanamama wa Tanzania ndoo kichwani, sasa ni muhimu tukazingatia hili na Mhandisi asiyekuwa na uwezo wa kazi aondolewe tuwaache wenye uwezo,” Waziri Aweso alisisitiza.

RUWASA inafanya kazi katika mikoa 25 ya Tanzania.

Michael K. Williams afariki Dunia
Maadhimisho siku ya wazee