Ambwene ‘AY’ Yesaya amekuwa mhanga mwingine wa kufungiwa kwa kazi za wasanii wa muziki nchini zinazodaiwa kukiuka maadili, baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kuzuia vituo vya runinga kuonesha video ya wimbo wake ‘Zigo Remix’ aliomshirikisha Diamond.

AY ameonesha kusikitishwa na hatua hiyo ya TCRA ambayo hakuitarajia na kueleza namna ambavyo alizipata taarifa za kufungiwa kwa wimbo wake.

AY Zigo

“Mimi niliona Mamlaka ya Mawasiliano TCRA, nilitumiwa copy ya barua na kati ya marafiki zangu wa karibu ambaye anafanya kazi katika media houses… akanitumia na nikaona imeandikwa ‘Zigo’ haina maadili,”AY ameiambia Clouds Fm.

“Sijaelewa ni maadili gani kwa sababu kama maadili niliyoyakosea mimi ni ya kushoot kwenye swimming pool na kwasababu kwenye swimming pool watu sijawavalisha jeans na sijawavalisha matundubali na wamevaa nguo za swimming pool hapo kweli nitakuwa nimekosa maadili,”

Alisema kuwa yeye alishoot video hiyo kulingana mazingira ya eneo husika lililotumika, “huwezi kuvaa suti jangwani au huwezi kuvaa overall kwenye swimming pool.” Aliongeza.

AY alionesha kushangazwa na uamuzi wa TCRA kufungia nyimbo na video za Tanzania huku ikiziacha kazi za wasanii wa nje zikiendelea kuchezwa kwenye vituo vya runinga nchini.

“Kama unafungia wimbo wangu wa Zigo na kuacha video za akina Nicki Minaj ni sawa, kama wanaona maadili ya kina Nicki Minaj yako sawa na ya AY ndio yanavunja inabidi tu kukubaliana nao,” alieleza.

Naye Msemaji wa TRCA, Innocent Mungi alieleza kuwa

“Tumetoa taarifa kwenda kwa watangazaji wa vituo vya Televisheni ambapo sisi tunasimamia kanuni za utangazaji, zinaitwa kanuni za maudhui (contents regulation) za mwaka 2005, ambazo zimeainisha aina za maudhui yanayopaswa kuoneshwa hasa mchana ambapo watoto wanaangalia Televisheni,” alisema Mungi.

“Kwa hiyo taarifa ambayo imekwenda kwenye vyombo vya habari hasa Televisheni, sauti watu hawaoni aina ya watu wanaocheza, lakini inapotoka video ndio unakuja kuona kuwa yale maudhui yalipaswa kutoonekana hasa mchana,” aliongeza.

Alisema kuwa Mamlaka hiyo imetoa agizo kwa vyombo vyote vya habari hususan Televisheni kuzingatia kanuni za maudhui za mwaka 2005 kwa kuzingatia aina ya video zinazorushwa na vituo hivyo.

Video ya Zigo ilipata mafanikio makubwa tangu ilipotoka ambapo ilifikisha watazamaji zaidi ya milioni moja ndani ya wiki moja huku ikipewa nafasi za juu kwenye vituo vya Televisheni vya nje.

Taarifa ambayo Dar24 iliipata nyuma ya pazia kutoka kwa chanzo cha karibu cha wanamuziki AY na Diamond zinaeleza kuwa wimbo huo umepewa nafasi ya kuchezwa mara 45 kwa wiki kwenye kituo cha kimataifa cha TRACE.

 

Kifaru: Mtibwa Imepoteza Kwa Kuwakosa Wachezaji Wake Muhimu
Shilole atangaza kazi ya mwalimu wa kiingereza, Chukua namba yake hapa