Wanamuziki Ambwene ‘AY’ Yesaya na Hamisi Mwinjuma ‘FA’, wameweka pingamizi katika Mahakama Kuu dhidi ya Maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na Kampuni ya Simu ya Tigo dhidi ya maamuzi ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala yaliyotaka kampuni hiyo kuwalipa wasanii hao shilingi bilioni 2.18 kwa kutumia nyimbo zao bila ridhaa yao.

Wasanii hao ambao wanawakilishwa na wakili wao, Alberto Msando wamefika leo katika mahakama hiyo jijini Dar es Salaam kusikiliza muenendo wa shauri hilo. Mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya pingamizi hilo Juni 27 mwaka huu.

Akiongea na mtandao wa Bongo5, Wakili Alberto Msando alisema kuwa Mahakama Kuu imeshasikiliza pande zote kuhusu pingamizi waliloweka dhidi ya Tigo na Mahakama Kuu itatoa uamuzi wake Juni 27.

“Kichokuwepo leo ni kusikilizwa kwa mapingamizi ya awali ya maombi waliyoleta Tigo ya kuomba kwamba kuzuia kukaza hukumu iliyotolewa na mahakama ya Ilala. Kwahiyo leo tumesikilizwa mapingamizi hayo na mahakama itatoa maamuzi yake tarehe 27 mwezi wa sita kuhusu mapingamizi ambayo tumeyaweka dhidi ya maombi yao,” Alberto Msando, mwanasheria anayewawakilisha AY na Mwana FA aliuambia mtandao huo.

Naye mwanasheria Rosan Mbwambo wa kampuni ya Law Associates anayeiwakilisha Tigo, alisema kuwa hawajaridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala ndio sababu wameamua kukata rufaa Mahakama Kuu.

Nyimbo ambazo wasanii hao wa Bongo Flava wanadai Tigo walizitumia bila ridhaa yao kwenye miito ya simu ni ‘Dakika Moja’ na ‘Usije Mjini’.

Lady Jay Dee amuandikia barua nzito Gardner, Ampa nafasi ya Mwisho
Picha: Magaidi wa ISIS wawaua mashabiki wa Real Madrid Kikatili