Rapa mahiri kutoka kwenye kiwanda cha muziki wa bongo fleva, Ambwene Yesaya ‘AY’ amedokeza ujio wa wimbo mpya atakaoshirikiana na mwanamuziki nyota wa miondoko ya Singeli, Sholo Mwamba.

AY, ameutumia ukurasa wake wa mtandao wa twitter kuwaarifu mashabiki wake kuhusu ujio wa wimbo huo ambao kwa mujibu wa chapisho utatoka siku chache zijazo, na kugusa hisia za idadi kubwa ya mashabiki wenye shauku kubwa ya kuusikia.

Maswali ya wengi yakiwa ni Je, rapa huyo ameimba Singeli, au atapita vipi kwenye mdundo wa Singeli kutokana na kuzoelekeka kwenye miondoko ya muziki wa rap zaidi.

Ambwene Yesaya ‘AY’ Picha na | AY/Instagram

kwa upande wa pili, chapisho la rapa huyo kushirikiana na mwanamuziki wa Singeli ambao ni muziki wenye asili ya Tanzania, limedhihirisha kiwango cha uzalendo ambacho amekuwa akikisisitiza mara kadhaa hasa akiwataka wasanii wa Tanzania kushiriki kunyanyua muziki wenye asilia ya Tanzania.

Miezi michache iliyopita, rapa huyo alipaza sauti akiwapinga wasanii wenye kujikita katika kufanya muziki wa ‘Amapiano’ ambao ni muziki wenye asili ya Afrika ya kusini, na kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya kuacha utamaduni huo, licha ya madai ya wasanii wengi kuzingatia biashara na kufuata ‘Trends’.

“Sisi tunajenga bongo fleva, wao wana Amapiano, Nigeria wana muziki wao, umeshawahi kuona Mnigeria anaimba wimbo wa South Afrika ?, HAPANA, Kama wasanii wanadai ni biashara ya muziki, Kwanini wewe unakuwa unawafuata watu, watu wasikufuate wewe?.

Ambwene Yesaya ‘AY’ Picha na | AY/Instagram.

“Sisi kufanya muziki wa mataifa mengine ni sawa na kumsaidia jirani kujenga nyumba yake wakati hujamaliza kujenga ya kwako, mwisho wa siku nyumba yake itaisha na atakufungia nje tu” alisema AY.

AY ft Sholo Mwamba, hii itakuwa rekodi ya pili kutoka kwa rapa huyo tangu kuanza kwa mwaka 2022, baada ya rekodi ‘Master’ alioutoa mapema mwezi Machi akiwa ameshirikiana na mwanamuziki nguli wa muziki wa bongo fleva Juma Nature.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 24, 2022
Sensa: Tulia awatoa hofu Watanzania maswali ya Makarani