Klabu ya Azam FC imepania kuuboresha Uwanja wake ili kukidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ sambamba Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Uwanja wa Azam Complex ni miongoni mwa viwanja bora ndani ya Afrika Mashariki na umekua ukitumiwa na Klabu mbalimbali za za ukanda huo pamoja na Timu za Taifa ya Tanzania.

Mhandisi wa Uwanja huo, Victor Ndozero amezungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu (Novemba 28) majira ya mchana na kusema, wanatarajiwa kuweka viti kwa mashabiki na kuondoa kabisa mbao ambazo zinakaliwa kwa sasa.

Ndozero amesema viti hivyo tayari vipo bandarini na kilichobaki ni kuanza kuviweka ili wakidhi vigezo vya kimataifa.

“Tunaweka viti takribani 10,000 na hivi ni kwa mashabiki wanaokaa kwenye mabenchi kule ili kufikia levo ya FIFA na CAF,” amesema Ndozero na kuongeza;

“Viti hivyo vitakuwa na rangi ya machungwa, Nyeusi, Nyeupe na Bluu, hakuna tena shabiki ambaye atasiamama akija kuangamia Michezo yetu na Michezo ya timu zitakazocheza hapa.”

Ndozero amesema leseni ya uwanja wao inamalizika mwishoni mwa mwaka huu na wanataka itoke leseni nyingine ambayo itakuwa kubwa zaidi.

“Tunataka timu za Afrika nzima zikifungiwa viwanja vyao basi wafikirie kuja hapa Chamazi na ndio lengo letu.”

Victor ameongeza akisema utaratibu wa uwekaji viti hivyo utaanza pindi timu yao (Azam) itakapokuwa inacheza mechi za nje ya Chamazi.

“Ndani ya wiki mbili tunaweza kuweka viti 2000 hadi 3000 na mzunguko wa pili kabla haujaanza tutakuwa tumemaliza.”

Azam Complex ni uwanja wa sita wenye nyasi bandia nchini sambamba Kaitaba (Bukoba) na Uhuru (Dar), Nyamagana (Mwanza), Black Rhino (Karatu) na Majaliwa (Ruangwa).

Uwanja huo ulianza kutumika rasmi 2010 na kuingiza mashabiki 10,000.

Wachezaji Young Africans wapigwa marufuku
Mayele atangaza njaa ya mabao Ligi Kuu