Baada ya kuandaa kwa mafanikio michuano ya vijana ya Afrika Mashariki ‘Azam Youth Cup 2016’ iliyomalizika jana, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, sasa inatarajia kuandaa michuano mikubwa zaidi ya vijana barani Afrika.

Michuano hiyo iliyoshirikisha timu nne kwa kuanzia mbili kutoka Tanzania, wenyeji Azam FC Academy na Future Stars Academy (Arusha) pamoja na timu za nje ya nchi Ligi Ndogo Academy (Kenya) na Football for Good (Uganda).

Azam FC Academy ndio wameibuka mabingwa, Football for Good ya pili, Ligi Ndogo iliyotoa nyota kadhaa wanaotamba nchini Kenya kama vile mshambuliaji hatari Jesse Were na Victor Wanyama anayetamba nchini Uingereza katika klabu ya Southampton yenyewe imekamata nafasi ya tatu huku Future Stars ikiwa ya nne.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz wakati wa ufungaji wa michuano hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa michuano hiyo ya vijana itakayoshirikisha timu mbalimbali kubwa za Afrika itafanyika Desemba mwaka huu na kushirikisha takribani timu 16.

“Dhamira kubwa ya Azam ni kuendelea kulea vipaji vyetu, kijana unapokuwa unampa mazoezi huwa anajipima kwa ajili ya mashindano, hapa nyumbani kulikuwa na mashindano ya vijana ya Uhai Cup, lakini sasa hayapo tena na hiyo imetuathiri sisi, hivyo tukaangalia tutafute njia gani ya kuhakikisha vijana wanacheza kwani tulikuwa haturidhiki na mechi za utangulizi za ligi wanazocheza na ndio tukaamua kuja na michuano hii.

“Na tumefanya michuano hii kwa kuanzia tu tukiwa na timu nne, lakini mapokeo yamekuwa ni mazuri, wachezaji wamefurahi, mashabiki waliojitokeza nao wameridhika kiasi ambacho watu wamekuwa wakituambia kwa nini isingekuwa ni ligi ya mikondo miwili ili waendelee kuona mechi zaidi, lakini tayari sisi kwenye maandalizi yetu tulikuwa tumejipanga kwa ajili ya mechi hizo tu,” alisema

Kawemba aliwaahidi mashabiki wa timu hiyo kuwa michuano hiyo ya Afrika Mashariki itakuwa endelevu na itafanyika tena mwakani katika kalenda kama hii kwa timu kuongezeka zaidi, huku akisisitiza kuwa watapata burudani nyingine ya soka la vijana Desemba mwaka huu kwa kushuhudia michuano mikubwa zaidi ya Afrika.

“Tunatarajia kuwa mwakani yatakuwa ni mazuri zaidi ya haya, mapungufu yaliyojitokeza mwaka huu yatafanyiwa kazi, lakini tunachowamba zaidi mashabiki na wapenzi wa mpira wale ambao wanahusika na soka la vijana, waone ya kwamba kitu kama hiki kinawezekana…Mbali na mpira tumeweza kufanya vikao na wamiliki wa vituo vyote na kujadili maendeleo ya soka la vijana Afrika Mashariki na changamoto zinazotukumba, hivyo tumepata kitu ambacho ni kizuri zaidi,” alisema.

Awashukuru Wakurugenzi Azam

Bosi huyo aliyebobea kwenye mambo ya uongozi wa soka, alisema kuwa wataendelea kusapoti soka la vijana huku akiwashukuru Wakurugenzi wa Azam kwa kufanikisha uandwaaji wa michuano hiyo pamoja na Kampuni ya Azam TV kwa kuwapa fursa Watanzania kuyashuhudia moja kwa moja kwenye luninga zao.

“Kubwa zaidi tunawashukuru Wakurugenzi wetu wa klabu na Kampuni ya Bakhresa kwa ujumla kwa sababu mashindano haya yameandaliwa kwa asilimia 100 na klabu ya Azam, kwa hiyo isingekuwa jitihada zao na ridhaa yao tusingeweza kupata pesa ya kuweza kuandaa michuano hii, hivyo tunapenda kuyakaribisha makampuni mengine huko mbeleni yaweze kushirikiana nasi tutakapoandaa michuano mikubwa zaidi na nafasi ipo kwao,” alisema.

Mbali na tuzo ya kombe la ubingwa walilopata Azam Academy, pia baadhi ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye kila idara waliweza kupewa tuzo binafsi kufuatia mafanikio hayo, ambapo mshambuliaji hatari wa timu hiyo Shaaban Idd, aling’ara kwa kutwaa tuzo mbili ya Ufungaji Bora kwa mabao yake matano pamoja na ile ya Mshambuliaji Bora wa mashindano.

Tuzo ya Beki Bora ilienda tena kwa beki wa Azam Academy, Abas Kapombe, ambaye ni mdogo wa staa wa Azam FC, Shomari Kapombe, kufuatia kiwango kizuri alichokionyesha kwenye michuano hiyo.

Football for Good Academy nayo iling’ara kwa kutoa wachezaji wawili waliotwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa michuano hiyo, aliyoitwaa Stephen Bongomin na nahodha wake Allan Ganukupa, akitwaa Tuzo ya Kiungo Bora huku Tuzo ya Kipa Bora ikienda kwa kipa wa Ligi Ndogo Rodgers Siteti.

Video: Hauhitaji Kwenda Nje ya Nchi - Salehbhai Glass Industries Ltd
Liverpool FC Yapanga Kumsajili Kieran Gibbs