Maafande wa jeshi la kujenga taifa (JKT Ruvu) leo jioni watashuka dimbani kumenyana na Azam FC katika mchezo wa kujipima nguvu utakaofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex saa 10 jioni huku wakitamba kutisha katika mchezo huo.

Maafande hao ambao wanafanya mazoezi katika uwanja wa JKT Mbweni ambapo ndio wameweka kambi kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania bara itakayoanza Agosti 20 utakuwa ni mchezo wao wa kwanza mkubwa wa kujipima nguvu.

Afisa Habari wa klabu hiyo Constantine Masanja ameiambia Dar24.com kuwa wachezaji wote wako vizuri na wanasubiri kwa hamu kubwa kufunguliwa kwa pazia la ligi ili waweze kuwaonesha wapenzi wa timu hiyo jinsi ya kusakata kandanda.

“Wachezaji wote wako timamu kwa ajili ya mchezo wetu na Azam FC na wameahidi kuibuka na ushindi ili kuziwashia taa ya nyekundu timu zinazoshiriki ligi kuu msimu ujao,”alisema Masanja.

Kikosi cha Maafande hao kipo chini ya kocha msaidizi Azishi Kondo huku wakimsubiri kocha mkuu Malale Hamsini ambaye muda wowote atajiunga nao baada ya kumaliza kozi ya ukocha wa leseni A hatua ya kwanza inayotolewa na shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Msimu uliopita Maafande hao walikuwa wakinolewa na kocha Abdallah Kibaden ‘Mputa’ ambaye sasa amepandishwa cheo na kuwa mkurugenzi wa JKT Ruvu.

Alberto Moreno Amrudisha Sokoni Jurgen Klopp
Basata Yamtosa Ney Wamitego