KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa mkoani Kigoma wikiendi hii Jumamosi (Desemba 3, 2016) kusaka vipaji vya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17).

Huo ni mwendelezo wa mpango wa Kitaifa wa timu hiyo wa kutengeneza kikosi imara cha timu ya vijana wa umri huo, ambapo inakwenda Kigoma kutokana na mkoa huo kuwa historia ya kisoka nchini ya kutoa wanasoka wengi waliotamba.

Majaribio hayo ya pili kuelekea mwisho wa kufungwa zoezi hilo, yatafanyika ndani ya Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Jumamosi hii kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na vijana wanaotakiwa ni wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2000 hadi 2004.

Mpaka sasa zoezi hilo limeshahusisha mikoa sita, ambayo ni Dar es Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Visiwani Zanzibar, Mbeya na Mwanza, ambapo kiujumla Azam FC imewafanyia usaili jumla ya vijana 3, 265 na kuvuna 70 pekee kati ya hao waliochaguliwa, huku 151 wakiwekwa akiba kwenye kumbukumbu za mradi huo.

Vijana hao wote waliochaguliwa kwenye mikoa mbalimbali, wanasubiria kuitwa kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex baadaye mwezi huu Desemba, ambao ndio utatoa vijana bora watakaounda timu hiyo.

Mapya Yaibuka Kuhusu Langa Lesse Bercy, TFF yanena kuhusu tetesi za kifo chake
Video: Sakata la kufungwa kiwanda cha Dangote, Waziri Mwijage ataka asiingiliwe