Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa upo kwenye mchakato wa kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni nia ya dhati kabisa ya Azam FC kutaka kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa inayokuja kuanzia mwezi ujao na mwakani (Kombe la Kagame na lile la Shirikisho Afrika).

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu, tayari wamemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wakijikusanyia jumla ya pointi 25, wakizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejizolea 35.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz juzi Kocha Msaidizi wa Azam FC, Yeray Romero, alisema kuwa kuelekea mzunguko wa pili wa ligi wanatarajia kuangalia mapungufu ya kikosi hicho kabla ya kuingiza sura mpya kwenye usajili ya dirisha dogo kwa ajili ya kuinyanyua timu na kufika kwenye nafasi nzuri zaidi.

“Wakati wachezaji wapya wanaingia pia tunatarajia kuwaangalia wachezaji ambao tunadhani kwa sasa kikosini hawawezi kuisaidia timu, ambao ndio watawapisha wachezaji hao, lengo la yote haya ni kuweza kuipeleka mbele zaidi timu zaidi ya hapa ilipo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Romero aliwapongeza wachezaji kwa kazi waliyoweza kuifanya mpaka sasa huku wao kama benchi la ufundi wakiahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa asilimia 100 katika kuirekebisha zaidi timu na kuziba mapungufu yaliyopo.

Video: Mwili wa Samuel Sitta wawasili Karimjee kwa ajili ya kuagwa
Diego Costa Kuikosa England