Klabu bingwa  Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho Jumapili itarusha karata yake ya kwanza muhimu kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, pale itakapowakaribisha Esperance ya Tunisia katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ipo fiti kabisa kuelekea mchezo huo, lakini itaingia dimbani ikiwa bila nyota wake wawili beki Shomari Kapombe na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao ni wagonjwa.

Kapombe hivi sasa bado yupo nchini Afrika Kusini akiendelea na vipimo kwa ajili ya kubaini tatizo linalomsumbua kutokana na kubanwa mbavu huku Sure Boy akisumbulia na mjeraha ya nyonga aliyoyapata wakati wa mchezo wa Ndanda.

Akizungumza mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema licha ya kuwakosa nyota wake hao amejipanga kuja na mfumo mpya utakaowawezesha kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Esperance.

“Nitawakosa Sure Boy na Kapombe kwenye mchezo wa kesho, Sure Boy anahitaji mapumziko ya siku nne ili kurejea kwenye hali yake ya kawaida, kwa Kapombe bado haijajulikana kwani hivi sasa tunasubiria ripoti kutoka Afrika Kusini kujua maendeleo ya afya yake.

“Nitakuja na mfumo mpya kwa ajili ya kupambana na hali hiyo ambao utaanza tukiwa na mabeki wanne ambao utakuwa ni mzuri wa kupambana na mfumo wa 4-2-3-1 wanaotmia wapinzani wetu, hivyo mabeki wa pembeni wataanza Erasto Nyoni na Wazir Salum, pengo la Sure Boy litazibwa na Messi (Ramadhan Singano), atakayecheza kama namba 10,” alisema.

Hall alisema amelenga ushindi kwenye mchezo huo na kudai kuwa atapanga kikosi chenye muonekano wa kushambulia zaidi kwenye nafasi za mbele ukiondoa viungo wawili wa ukabaji watakaokuwa wakiwasaidia mabeki kutimiza majukumu ya kukaba.

Waarabu Walazimisha Sare Dar es salaam
Ridhiwani 'anawa mikono' sakata la ufisadi wa Mabilioni ya Jeshi la Polisi