Uongozi wa Azam FC unaamini mchezo wa jana Jumatano (Mei 18) kikosi chao kilikua na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na kiwango kizuri kilichoonekana ndani ya dakika 90.

Azam FC waliokua nyumbani Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam, walipata bao la kuongoza kupitia kwa Mshambuliaji wao kutoka Zambia Rodgers Kola, lakini dakika chache baadae Simba SC ilisawazisha kupitia kwa Nahodha na Mshambuliaji John Bocco kipindi cha kwanza.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo yenye Maskani yake Makuu Chamazi jijini Dar es salaam Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema, kwa hakika wachezaji wao wameonesha thamani ya Azam FC kwenye mchezo huo ambao walikaribi kuibuka na alama tatu muhimu.

“Mchezo wa soka hutoa nafasi kwa yoyote kushinda, nadhani sisi tulistahili kushinda mchezo huu, kwa sababu tulimiliki kwa kiasi kikubwa na tuliwaweza Simba SC katika kila idara, hivyo walichokipata ni kama bahati kwao.”

“Ilikua muhimu sana sisi kushinda kwa sababu kuna kitu tunakitafuta katika kipindi hiki cha mwishoni mwa msimu, lakini naamini bahati haikuwa kwetu na ndio maana ninakiri kuwa Simba SC wamebahatika kupata sare.”

“Lakini pia tunapaswa kufahamu kuwa ilikua ngumu kuifunga Simba SC kwa sababu walijua namna ya kukabiliana na mitego yetu, pia uzoefu wao umewasaidia sana kwa sababu wameshiriki vizuri kwenye michuano ya Kimataifa, kwa hiyo matokeo ya sare bado yanasimama kwenye bahati yao.” amesema ‘Zakazakazi’

Kwa matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC, Simba SC imefikisha alama 50 zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Young Africans ikiwa kileleni kwa kumiliki alama 60.

Azam FC imefikisha alama 33 ambazo zinaiweka klabu hiyo ya Chamazi jijini Dar es salaam katika nafasi ya tano, ikitanguliwa na Geita Gold FC yenye alama 34 na Namungo FC yenye alama 36.

28 wafariki wakigombea mifugo
Zakazakazi: Kwani hakuna waamuzi wengine?