Benchi ufundi la klabu bingwa ya Afrika mashariki na kati Azam FC, limesema kuwa hawatabweteka na matokeo mazuri ya awali waliyopata ugenini dhidi ya Bidvest Wits badala yake watapambana hadi dakika ya mwisho kuelekea mchezo wa marudiano Jumapili ijayo (Machi 20).

Azam FC inayodhaminina na Benki ya NMB ambayo ni bora kabisa nchini Tanzania, ilirejea nchini jana saa 12.15 ikitokea jijini Johannesburg, Afrika Kusini ikiwa na ushindi mnono wa mabao 3-0 mkononi iliyoupata dhidi ya Wits katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya marudiano itapigwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 9.00 Alasiri.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (dk 51), Shomari Kapombe (dk56) huku nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akitupia msumari wa mwisho dakika ya 59.

Kabla ya mchezo huo wa marudiano, Azam FC keshokutwa Jumatano itashuka tena dimbani kuvaana na Stand United katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alisema kuwa wanatakiwa kuwa waangalifu na kujua mbinu watakazokuja nazo wapinzani wao na namna watakavyouchulia mchezo huo wa marudiano.

Alisema tokea mwanzoni mwa mwaka huu waliposhiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, walijua ya kuwa wanaenda kucheza na Bidvest Wits, hivyo hadi wanafanikiwa kudhibiti mbinu zao wamefanikiwa kuwasoma kwenye mechi takribani sita, tano kupitia DVD na moja wakiwaangalia ‘live’ nchini Seychelles walipocheza na Light Stars.

“Hatuwezi kuanza kufikiria kuwa tayari tumeshavuka kufuatia ushindi huo, kwenye mpira huwezi kusonga mbele kabla ya dakika ya mwisho ya mchezo wa mwisho, hivyo pia tunatakiwa kujua ni wachezaji gani watakaopatikana baada ya mchezo wa Jumatano (Stand United) tunaye mtaalamu wa viungo ambaye atatuambia yupi mchezaji ana matatizo ambaye hatakuwepo kwenye mchezo huo wa marudiano,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo wa kwanza, Mario alisema wachezaji wote walifanikiwa kuonyesha viwango vizuri uwanjani kwa kupambana na kucheza kupitia mbinu walizowafundisha kukabiliana na wapinzani wao huku akidai kuwa Azam FC ni timu bora kabisa na walifanikiwa kuonyesha ubora wao kwenye mchezo huo.

“Ni ngumu kusema sehemu gani ilicheza vizuri, kitu ninachoweza kusema kila sehemu ilifanikiwa kucheza vizuri kuanzia kwa Aishi (Manula) langoni, sehemu ya ulinzi, kiungo na hata eneo la ushambuliaji, kilikuwa ni kiwango kizuri usiku huo kwa kweli kwa timu yetu.

“Kikubwa sisi kama benchi la ufundi tuliweza kujua ubora wao wa kutumia mipira ya adhabu ndogo na krosi na hatukuwapa mwanya huo, tulicheza kwa staili yetu na tulimiliki mpira na kuwanyima mpira wao hii iliwapa wakati mgumu kwenye mchezo huo na kweli mbinu yetu ilifanikiwa,” alisema.

Awapongeza waamuzi?

Kocha huyo raia wa Romania, aliwapongeza waamuzi waliochezesha mchezo huo kutoka nchini Madagascar kwa kuonyesha kiwango bora kabisa bila kupendelea upande wowote huku akidai kuwa Tanzania inapaswa kuiga uchezeshaji ule.

“Watu wanaweza kusema kwa nini Azam FC haionyeshi kiwango kile kizuri Tanzania, nilisema awali kuwa Tanzania Azam FC haitakiwi icheze mpira kwa sababu ya waamuzi kwani wanafanya vitu vya aibu uwanjani, hivyo hatuwezi kucheza aina ya soka tunalotaka kucheza

Urejeo wa Aggrey Morris?

Kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje ya dimba kwa takribani miezi mitatu akiuguza majeraha ya goti, beki kisiki wa Azam FC Aggrey Morris alirejea dimbani dhidi ya Bidvest na kuliongoza eneo la ulinzi kutoruhusu bao lolote kutoka kwa wapinzani wao.

“Ametoka kwenye majeraha makubwa na ameonyesha kiwango kizuri leo (Jumamosi) ni ngumu kusema alikuwa mchezaji bora uwanjani, lakini ni mmoja wa wachezaji waliowadhibiti wachezaji wa Bidvest na sisi kutofungwa bao ugenini,” alisema Mario.

Mechi vs Stand United?

Kuelekea mchezo dhidi ya Stand United, alisema kuwa jambo la kwanza wataangalia wachezaji waliofiti kuelekea mchezo huo huku akitanabaisha kuwa lengo lao ni kupata ushindi katika mchezo huo ili kuendeleza mbio za kuwani ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

 

 

Antonio Conte Ajiweka Njia Panda
Muro Amjibu Haji Manara Kwa Kumtaka Ajivunie Historia Yake