Benchi la ufundi la Azam FC limejinadi kukamilisha kazi ya kukiandaa kikosi cha klabu hiyo, tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania FC.

Mchezo huo utachezwa leo saa moja usiku Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, huku kila upande ukiamini upo katika mazingira mazuri ya kuanza msimu kwa kuzinyakua alama tatu muhimu.

Akizungumza kwa niaba ya benchi la ufundi la Azam FC kocha msaidizi Vivier Bahati, amesema kikosi chao kipo vizuri, na kinasubiri muda wa pambano ili kuonyesha namna walivyodhamira kufanya vyema msimu huu.

Kocha Vivier amesema kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania pamoja na michezo mingine ya msimu mzima.

“Kiujumla ligi itakuwa ni ngumu, tumejiandaa kutafuta alama (Pointi) muhimu katika kila mchezo, tunawaheshimu wapinzani wetu, tumejipanga kutafuta matokeo kwa kila mechi ili kufikia malengo yetu,” amesema kocha huyo kutoka nchini Burundi.

Kwa upande wa Kocha wa Polisi Tanzania FC, Malale Khamsini amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kutafuta alama muhimu katika mpambano dhidi ya Azam FC.

“Tumejipanga, vijana wangu wana ari ya kufanya vizuri, tunacheza usiku hivyo  haitakuwa kigezo kwetu kupoteza pointi, tunawaheshimu Azam wamefanya usajili mzuri lakini hata sisi tumeboresha timu yetu,” amesema Malale.

Amesema muda wa usiku ambao mchezo utachezwa haitawaathiri na kuzuia kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wanaocheza ugenini.

Michezo mingine ya Ligi Kuu inayochezwa leo Jumatatu (Septemba 07) itashuhudi Kagera Sugar wakiwakaribisha JKT Tanzania, kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba saa kumi jioni, na jijini Dar es salaam KMC FC watakua wenyeji wa Mbeya City kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es salaam kuanzia mishale ya saa nane mchana.

Msimu wa 2020/21 ulianza rasmi jana kwa michezo sita kuchezwa kwenye viwanja tofauti.

E.F.A waanza msako wa mataji
Wanaojitokeza tokeza wataisoma namba - Magufuli