TIMU ya Azam FC leo imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, la kufanya usafi siku ya kumbukumbu ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Azam FC katika kutekeleza agizo hilo, leo majira ya saa 12.30 asubuhi ilitembelea Zahanati ya Chamazi na kufanya usafi kwa muda wa takribani saa mbili na nusu.

Wafanyakazi mbalimbali, viongozi pamoja na wachezaji wa Azam FC, walishiriki zoezi hilo, ambapo watu mbalimbali wanaoishi maeneo karibu na zahati hiyo walionekana kufurahia kitendo hicho kilichofanywa na timu hiyo.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa wanamshukuru Mungu baada ya jambo hilo walilokuwa wamelipanga kufanikiwa.

“Tulilipanga jambo hili katika siku ambayo Rais John Pombe Magufuli aliposema leo (siku ya Uhuru) itakuwa ni usafi, tukaona ya kwamba tunajukumu Azam FC kuona tunshiriki katika kampeni hiyo na tukaangalia ni wapi tunaweza kwenda, tukaona tuje kwa majirani zetu hapa badala ya kwenda shule au sokoni.

“Kwani ni sehemu tunayopita kila siku na kwa majirani zetu, tukaona haturidhiki na hali ambayo tunaiona kila tukipita hapa, tukasema itakuwa ni busara kama tukija kufanya usafi eneo hili na tunashukuru tulipouona uongozi wa Zahanati, walitupokea na kuahidi kutupa ushirikiano na kweli leo toka saa 12.30 asubuhi tulipofika hapa wametupa ushirikiano mkubwa,” alisema.

“Tunashukuru shughuli yetu imekwenda vizuri na katika kiwango tulichokuwa tumekitarajia, na nafsi yetu ikasema ya kwamba tumejitolea kwenye jamii, ukizingatia ya kwamba Azam inacheza mpira na tunapocheza mpira tunacheza na mashabiki.

“Na maeneo tuliyopo, hospitali ambayo inahudumia ni hii hapa ya Chamazi na sisi tuko eneo hili na mashabiki wetu wanapokuja uwanjani wanatakiwa kuwa na afya njema na wakiugua watakuja hapa kutibiwa,” alisema.

Kawemba aliwaomba mashabiki wao popote pale walipo wafanye tukio kama hilo na kuongeza kuwa linatakiwa kuwa endelevu, huku kudai watakapohitajika eneo jingine lolote kwa wakati mwingine wakafanye hivyo hawatasita kwenda.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Zahanati hiyo, Mohamed Hassan, aliipongeza na kuishukuru sana Azam FC kwa kufika kwenye hospitali yao na kufanya usafi.

“Azam wanatabia kwanza ya kuangalia maeneo yao ya majirani kama sisi vile, wameangalia maeneo yao ya jirani na kuona hawana sababu ya kwenda sehemu nyingine kwa kuwa wanapita hapa na wachezaji wao wakiugua watawaleta hapa.

“Kwa hiyo wakaona tuipe kipaumbele Zahanati ya Chamazi, sisi tunawapongeza sana, huu ni ushirikiano mzuri baina yetu,” alisema.

Hassan aliongeza kuwa: “La pili Azam na sisi tumeitikia wito wa Rais Magufuli kwamba tufanye kazi na tuache mambo ya kwenda kule na tutengeneze usafi na huu usafi unaashiria ya kuwa magonjwa ya milipuko yanaweza kuondoka.”

Naye mmoja wa wachezaji wa timu ya Azam FC Academy, Salim Juma, alisema wanajisikia furaha sana wao kama wachezaji kuwajibika kufanya usafi ili kuhakikisha usafi unatawala katika nchi yetu.

“Mimi natoa wito kwa vijana wengine tuje tushirikiane ili kuhakikisha tunalisafisha jiji letu, kwani kusafika kama ni ubora tunaupata wote, sote tutanufaika na jambo hili, magonjwa ya mlipuko madogo na makubwa hayatakuwepo,” alisema.

Tyson Fury Apokonywa Ubingwa Wa Dunia
Msichana aliyechukuliwa na Justin Bieber ageuka Mwehu, Polisi watinga hotelini