Uongozi wa Azam FC umeshangazwa na taarifa za kuendelea kuhusishwa na Mpango wa kumsajili Kiungo wa Young Africans Feisal Salum ‘Fei toto’.

Azam FC imekuwa ikihusishwa na usajili wa kiungo huyo kutoka Zanzibar kwa majuma kadhaa, huku ikielezwa tayari imeshatenga fungu maalum kwa ajili ya kuvunja mkataba wake Young Africans.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdul-Karim Amin ‘Popat’ amesema hakuna ukweli wowote kuhusu usajili wa Kiungo huyo, ambaye kwa sasa amekuwa akifanya vizuri.

Amesema taarifa hizo hizo ni tetesi kulingana na ubora anaouonesha mchezaji huyo ili kujitengenezea njia ya kupata Donge nono kutoka kwa waajiri wake, wakati mkataba wake ukielekea ukingoni.

Popat amesema uwezo na kiwango cha nyota huyo ni kizuri lakini kwa sasa kikosi cha Azam FC kiko kamili kupambana ili kutimiza malengo yake.

“Sisi timu yetu inajitosheleza, Feisal ni mchezaji mzuri lakini hatuna mpango naye, hizo ni tetesi tu na ni njia za wachezaji kutengeneza mipango ya kupata pesa nyingi zaidi kwenye vilabu vyao, pindi ya mikataba inapoelekea ukingoni.”

“Mchezaji yeyote akiwa kwenye kiwango bora, haya mambo yanaibuka kwa kutengenezwa na mameneja wanaowasimamia wachezaji, na huo muda ndio wanatengeneza mazingira ya kujipatiwa pesa kupitia hawa wachezaji.”

Hata hivyo kauli ya Popat inakwenda kinyume na kauli aliyoitoa Kaimu Afisa Habari wa Azam FC Hasheem Ibwe alipohojiwa na vyombo vya habari jijini Dar es salaam.

Katika mahojiano hayo Ibwe amesema ndoto ya Azam FC ni kuwa na mchezaji Fei toto katika kikosi chake.

“Hakuna Timu ambayo haimtaki Feisal Salum kwenye Timu zote za ligi Kuu na sio ligi Kuu tu, Kenya, Uganda Afrika Mashariki na Kati mpaka ukanda wa SADC wote wanatamani kupata huduma ya Fei Toto.”

“Ni namba 10 ya viwango, ni namba nane ya viwango, ni kiungo ambaye anaweza kutoka pembeni. Azam FC kwanini tusiwe na furaha kuhusishwa na mchezaji wa hadhi ya juu Tanzania, kwa hiyo ni ndoto ya kila Timu ligi kuu na Sisi Azam ni ndoto yetu kuwa na mchezaji kama Feisal.” amesema Hasheem Ibwe

Mpinzani wa Ramaphosa uongozi ANC 'afungunga'
Juma Mgunda: Sitafanya mzaha Kombe la Shirikisho