Wababe wa Young Africans, KMC FC keshokutwa Jumatano watacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa kombe la shirikisho Tanzania bara (ASFC) Azam FC.

KMC FC wanajipanga kucheza mchezo huo, huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibamiza Young Africans mabao matatu kwa sifuri katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam.

Mabao ya KMC FC katika mchezo huo yalifungwa na Sadala Lipangile, Charles Ilanfya pamoja na Hassan Kabunda.

Kocha Mkuu wa KMC FC, Haruna Hererimana amesema wamepokea mwaliko kutoka kwa Azam FC wakiomba mchezo wa kirafiki utakaochezwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.

Kocha huyo amesema wamekubali mwaliko huo na anaamini kiosi chake kitaendelea kupata maandalizi mazuri kabla ya kuendelea kwa michezo ya ligi kuu Tanzania bara mwishoni mwa juma hili.

“Bado tutaendelea kutafuta michezo ya kirafiki hadi pale tutakapoona inafaa kupumzika na kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting.

“Tukimaliza kucheza na Azam tutaangalia mchezo mwingine mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo maana hatutaki kuwaacha wachezaji wetu wakae bila kucheza,” anasema Hererimana.

Kabla ya kutua KMC FC, Hererimana alikuwa akikinoa kikosi cha Lipuli FC na aliajiriwa klabuni hapo kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabovu.

TANESCO Mtwara yazidiwa na kasi ya wananchi kuunganisha umeme
Bundesliga wamlilia George Floyd