Wawakilishi wa Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ msimu ujao 2021/22 Azam FC, wamethibitisha kumsajili Kiungo Mkabaji kutoka nchini Zambia Paul Katema, akitokea Red Arrows.

Azam FC wamethibitisha usajili wa kiungo huyo, kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii leo mchana, ikiwa ni kama utaratibu wao kufanya hivyo katika kipindi hiki kila inapofika saa nane mchana.

Katema amejiunga na Miamba hiyo ya Azam Complex Chamazi, kwa mkataba miaka miwili ambao utadumu hadi mwaka 2023.

Katema ni miongoni mwa viungo bora nchini Zambia, hivyo anatarajiwa kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Kocha George Lwandamina ‘CHICKEN’ kwenye eneo hilo kuelekea msimu ujao.

Usajili wa Katema unakua watano kwa ajili ya msimu ujao, baada ya awali kusajiliwa kwa nyota wengine wawili kutoka Zambia, Charles Zulu, Rodgers Kola, Kenneth Muguna (Kenya) na Edward Manyama (Tanzania).

Azam FC itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu, kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21.

Msimu ujao Tanzania itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya CAF, ambapo Simba SC na Young Africans zitashiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Azam FC na Biashara United Mara zikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho.

Manara: Sijasambaza sauti mitandaoni
Shangazi mjumbe mpya bodi ya wakurugenzi Simba SC