Klabu ya Azam FC imeanza kuhusishwa na taarifa za kumsajili Mshambuliaji tegemeo wa Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal Omdurman, Mkongomani, Makabi Lilepo.

Azam FC imepanga kukisuka kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao ambao wanakwenda kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kusajili wachezaji wenye ubora na uzoefu na michuano hiyo ya kimataifa.

Mchezaji mwingine anayetajwa kuwaniwa na Azam FC ni mshambuliaji wa Marumo Gallants ya nchini Afrika Kusini, Ranga Chivaviro anayechuana na Fiston Mayele katika ufungaji kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika, wote wakiwa na mabao sita.

Taarifa zinaeleza kuwa Azam FC imehamia kwa Lilepo baada ya Young Africans kukaribia kufanikisha usajili wa Chivaviro, ambaye wakala wake wamekiri kuwa katika mazungumzo katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2022/23.

Imeelezwa kuwa baada ya Azam kuikosa saini ya Chivaviro, haraka mabosi wao wamepiga hodi Al Hilal Omdurman kwa ajili ya kuulizia mkataba wa nyota huyo, ambaye alifanya vizuri kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Azam FC imesitisha mipango yake ya kumsajili Chivaviro na sasa wamehamia kwa Lilepo ambaye ni kati ya washambuliaji bora na wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

“Kama mazungumzo yakienda vizuri na kufikia muafaka mzuri, basi upo uwezekano mkubwa wa kutumia gharama kubwa katika usajili kumpata Lilepo.

“Uongozi unataka wachezaji wenye uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa, kikubwa kufika katika hatua nzuri,” zimeeleza taarifa kutoka Azam FC

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ hivi karibuni alizungumzia mipango ya usajili ya timu hiyo, na kusema: “Tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji watatu ambao ni siri, hivi karibuni tutaweka wazi baada ya taratibu zote kukamilika, kati ya sehemu tutakazozifanyia maboresho ni ushambuliaji na beki.”

Kiongozi wa Mungiki apandishwa kizimbani, asomewa mashitaka
Serikali yaendeleza ufumbuzi changamoto za Muungano