Klabu ya Azam FC imetangaza njaa ya kusaka ushindi kwenye mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utawakutanisha dhidi ya Mbeya City, siku ya Alhamisi (Februari 18), Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.

Azam FC imetangaza njaa ya kusaka alama tatu muhimu za mchezo huo, baada ya kuambulia patupu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita jijini Tanga.

Katika mchezo huo Azam FC walikubali kichapo cha mabao 2-1, na kuendelea kuwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kubaki na alama 33 kibindoni.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa mipango yao ni kufanya vizuri kwenye mchezo iliyobaki ya Ligi Kuu, wakianza na Mbeya City siku ya Alhamisi.

“Kushindwa kupata matokeo kwenye mechi iliyopita haina maana kwamba hatupo imara, benchi la ufundi litafanyia kazi makosa kisha tutaendelea kusaka ushindi kwenye mechi zetu zijazo.” Amesema Thabit Zakaria.

Mbeya City iliyo nafasi ya 17 na alama zao 15, itakutana na Azam FC, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Young Africans, juzi Jumamosi (Februari 13).

Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza Mbeya City walikubali kufungwa bao 1-0 dhidi ya Aam FC, hivyo mchezo wa Alhamis Jumatano unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Kuagiza sukari nje mwisho 2022
Wakili wa Ruto aula ICC