Mabingwa wa kombe la shirikisho (ASFC) Azam FC kesho Ijumaa Novemba 08, 2019 watakua nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, wakiwakaribisha Biashara United waliofunga safari kutoka mjini Musoma mkoani Mara.

Azam FC watahitaji kuutumia mchezo huo vyema, baada ya kukwama katika harakati zao za kusaka alama tatu muhimu, mara tatu mfululizo, kufuatia kufungwa na mabingwa watetezi Simba SC, kisha Ruvu Shooting na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Azam FC Jaffar Iddy Maganga amesema maandalizi ya kuelekea mchezo huo muhimu, yameshakamilika chini ya kocha wao kutoka nchini Romania Aristica Cioaba akisaidiana na kocha mzawa Nassor Iddy Cheche.

Mchezo mwingine wa ligi kuu ya soka Tanzania bara utakaochezwa kesho ijumaa, utashuhudia Young Africans wakishuka dimbani kwa mara ya kwanza wakiwa chini ya utawala wa kocha wa muda Charles Boniface Mkwasa “Master”, ambaye amerithi mikoa ba Mwinyi Zahera alieonyeshwa mlango wa kutokea juzi jumanne.

Young Africans hiyo kesho watakua ugenini mkoani Mtwara wakipapatuana na Ndanda FC kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, na tarajio lao kubwa ni kudhihirisha mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu.

Kocha Mkwasa ambaye amewahi kuwa mchezaji na katibu mkuu wa klabu ya Young Africans, amesema hana budi kutumia mbinu chache kuelekea mchezo huo wa kesho kutokana na kuwa na muda mfupi wa kukiandaa kikosi chake, na anaamini atavuna matokeo mazuri dhidi ya Ndanda FC.

Kwa upande wa Ndanda FC ambao wamekua na matokeo mazuri kila wanapocheza nyumbani dhidi ya Young Africans, watakuwa na hitaji la kuendeleza rekodi hiyo kwa kuhakikisha wanaifunga timu hiyo kongwe hapa nchini na ikishindikana sana, basi angalau matokeo ya sare ambayo yatawabakishia alama moja nyumbani.

Video: ACT Wazalendo kukata rufaa wagombea wao kuenguliwa uchaguzi wa Serikali za mitaa
Meya nchini Bolivia akatwa nywele na kupakwa rangi