Kituo cha runinga cha Azam (Azam TV)  kimetoa ufafanuzi juu ya sakata la upotevu wa makontena 349 yaliyopotea bandari ambayo habari zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ziliezea kuwa baadhi ni za mmiliki wa kituo hicho, Said Bakhresa.

Upotevu huo wa makontena kwenye nyaraka za TRA ulibainika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kuagiza wote waliohusika kukamatwa na kuchukuliwa hatua sitahiki.

Kituo hicho cha runinga kimekanusha taarifa za zinazodai kuwa makontena hayo ni mali ya Bakhresa na kudai kuwa ukweli ni kwamba makontena hayo ni mali ya wafanyabiashara mbalimbali waliokuwa wametunza katika eneo la kuhifadhia makontena (ICD) linalomilikiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa.

Hivi ndivyo AZAM TV walivyoeleza:

“Uchunguzi wetu umeonesha kuwa si kweli kuwa kuna makontena zenye bidhaa zilizoingizwa na Kampuni hiyo (Bakhresa) kuwa miongoni mwa makontena yaliyohusika katika sakata hilo, isipokuwa kumetokea upotevu wa makontena yaliyoingizwa nchini na baadhi ya wafanyabiashara katika eneo la kuhifadhia makontena (ICD) linalomilikiwa na kampuni ya Bakhresa.

“Aidha, imebainika kuwa kuna uchunguzi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) huku kukiwa na ushirikiano na uongozi wa kampuni hiyo kuhakikisha wale wote wanaohusika na upotevu huo wanachukuliwa hatua na kodi yote ya serikali inalipwa na wamiliki wote wa makontena waliohusika na upotevu huo.

Waziri Mkuu alieleza kuwa Makontena hayo 349 yenye thamani ya shilinigi bilioni 80 yalionekana kwenye kumbukumbu za Bandari huku yakikosekana kwenye kumbukumbu za TRA, hivyo yalikwepa kulipa kodi kinyume cha sheria.

Majaliwa Aapa Kupambana Hadi Dakika Ya Mwisho
Walimu Wacharuka Kudai Stahiki Zao Sengerema