Mfadhili wa zamani mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Azim Dewji ameshangazwa na utaratibu aliouchukua msemaji mpya wa Young Africans Haji Manara.

Manara amekua na utaratibu wa kuisema vibaya Simba SC tangu alipojiunga na Young Africans mwezi Agosti, na amefanya hivyo mara kadhaa alipohojiwa kwenye vituo vya Radio na kuandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Dewji ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa mpango wa simba kucheza fainali ya michuano ya kombe la CAF mwaka 1993 amesema, anamsikitikia Manara kwa maamuzi aliyoyachukua ya kuhamia upande wa pili (Yanga) na kujibebesha jukumu la kuusema hovyo upande aliotokea.

Amesema hakupaswa kufanya hivyo na badala yake angefikiria kwenda juu zaidi kwa kuwania hata ubunge, kwani umaarufu alioupata akiwa Simba SC ungemuwezesha kuwashawishi wananchi na kumchagua.

“Namsikitikia Manara amekaa Simba na kupata umaarufu mkubwa sana, badala ya kutafuta ubunge au kitu kingine kikubwa ameishia kwenda Yanga, wakati alikuwa na nafasi kubwa ya kupata Ubunge”

“Huwezi ukakaa kwenye Klabu wakati wote, Kuna siku kitanuka tu. Lakini hatakama utaondoka iwe hata kwa mchezaji, inatakiwa utoke Klabu ndogo na kwenda Klabu kubwa, na siyo kutoka Klabu kubwa na kwenda Klabu nyingine kubwa inayolingana uwezo na Ile uliyotoka,”

” Pia amekua akisema hovyo kwa kudanganya kuhusu Simba SC, ninamshauri aache kwa sababu hakuna anaehangaika kujibu anachowaaminisha watanzania kuhusu alikotoka.” amesema Azim Dewji.

Manara aliondoka Simba SC mwishoni mwa mwezi Julai baada ya kuibuka kwa tafrani kati yake na afisa mtendaji mkuu Barbara Gonzalez.

Wachezaji wa Djibout wazamia Ufaransa
Kamwaga awashukia wanaoibeza TP Mazembe