Mfanyabiashara, Akram Azizi amepandishwa katika kizimba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka 75 yakiwemo ya uhujumu uchumi, ujangili, umiliki silaha kinyume cha sheria na utakatishaji fedha.

Azizi anatuhumiwa kukutwa na silaha 70, risasi 6,496 pamoja na kutakatisha fedha kiasi cha $9,018 (Sawa na Sh 20,653,023).

Mawakili wa Serikali Wakuu, Paul Kadushi na Faraja Nchimbi walimsomea mshtakiwa mashtaka 70 ya kukutwa na silaha, mashtaka mawili ya kukutwa na risasi, mawili ya kukutwa na nyara za Serikali pamoja na moja la utakatishaji fedha.

Baada ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile, hakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu na mtuhumiwa ataendelea kushikiliwa kutokana na kuwa na tuhuma za makosa ambayo hayana dhamana.

Kesi hiyo itasomwa tena Novemba 12 mwaka huu. Upande wa Mashtaka umeeleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Askari mwenye bunduki ndani ya chumba cha mtihani azua gumzo
Lugola ‘amsukuma ndani’ dereva wa basi aliyetaka kumsababishia ajali