Shirika la Afya Duniani (WHO) limefanya mkutano maalum kuangazia umuhimu wa kutambua na kufanyia kazi ugunduzi wa kirusi kipya cha Corona kilichogundulika nchini Afrika Kusini na kusema wataalamu mjini Geneva wataamua ikiwa kirusi hicho kinahitaji kutambuliwa kama ni hatari zaidi ya vyote vilivyopita.

Aina mpya ya kirusi cha Corona kinaitwa B.1.1.529 kilichogunduliwa hivi karibuni kina orodha ndefu ya mabadiliko ambayo yalielezewa na wanasayansi kuwa ni ya kutisha.

Visa vilivyothibitishwa bado vipo zaidi katika jimbo moja nchini Afrika Kusini, lakini kuna viashiria kwamba huenda virusi vya ugonjwa huo vikaenea zaidi na vinaarifiwa kuwapata zaidi vijana.

Hii leo nchi ya Ubelgiji imeripoti kisa cha kwanza cha aina hii mpya ya kirusi cha Corona barani Ulaya.

Kumekuwa na visa 77 vilivyothibitishwa katika jimbo la Gauteng nchini Afrika Kusini, visa vinne nchini Botswana na kimoja Hong Kong (ambavyo vinahusishwa moja kwa moja na watu kusafiri kutoka Afrika Kusini).

Hata hivyo, kuna dalili kwamba kirusi hicho kimeenea zaidi ya ripoti zinazotolewa na WHO inasema itatoa mwongozo mpya baada ya mazungumzo lakini imeonya kwamba itachukua wiki kadhaa kubaini kirusi hicho kinavyoweza kuambukizwa na ikiwa chanjo itasalia kuwa na ufanisi dhidi yake.

Tangu kutangazwa kugundulika kirusi hicho kipya cha Corona nchi kadhaa zimeweka vikwazo kwa mipaka ya nchi zao na hasa safari zinazotokea kusini mwa Bara la Afrika.

Ubelgiji imetangaza mgonjwa wa kwanza wa Kirusi hicho kipya na imesema kuwa safari zote za anga kwenda nchi zilizo na kirusi kipya cha corona zinapaswa kusitishwa.

Mapema leo Ujerumani, Italia na Uingereza zimejiunga na mataifa mengine ya Ulaya katika kuzuia safari za anga kutoka Afrika Kusini wakati mataifa hayo ya kupigania kujinusuru na kusambaa kwa aina mpya ya virusi.

Nchini Kenya wasafiri watakaoingia kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika lazima waoneshe uthibitisho wa kipimo cha PCR kinachoonesha kutokuwa na maambukizi na wakae karantini wanapowasili na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara baada ya hapo.

Waziri wa afya nchini Uingereza Sajid Javid ametangaza kuwa wasafiri wanaowasili nchini England kutoka mataifa tofauti ya Afrika watalazimika kujitenga na mataifa sita yataongezwa katika orodha, huku baadhi ya ndege zikipigwa marufuku kwa muda.

Kirusi hiki kipya cha Corona kimeacha wasiwasi mkubwa kuhusu, licha ya uelewa mdogo kukihusu wataalam wanasema ni moja ya virusi vinavyopaswa kuangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu na kuuliza maswali ya kina juu ya nini cha kufanya na wakati gani.

Somo kubwa kuhusu janga la corona ni kwamba huwezi kusubiri mpaka uwe na majibu yote na kila wakati unatakiwa kuchukua tahadhari.

RC Makalla:Jitokezeni kwa Wingi Sherehe za Uhuru
Mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi kupata Shahada ya Uzamivu (PHD) nchini Tanzania