Bingwa wa masumbwi ya uzito wa Welterweight anayeshikilia mkanda wa Chama cha Masumbwi Duniani (WBA), Keith ‘One Time’ Thurman alfajiri ya leo amefanikiwa kuutetea mkanda huo dhidi ya Josesito Lopez.

Thurman ambaye hajawahi kupoteza pambano hata moja akiwa na rekodi ya mapambano 29 ya kulipwa, alitawala pambano hilo licha ya Lopez kujaribu kuleta ushindani mkubwa.

Baada ya pambano, Thurman mwenye umri wa miaka 30 alieleza kuwa kinachofuata mbele yake angependa apande ulingoni dhidi ya bondia Mfilipino mwenye umri wa miaka 40, Manny Pacquiao ambaye hivi karibuni alishinda pambano lake dhidi ya Adrien Broner.

Keith Thurman akimshambulia Josesito Lopez

“Kama ikitokea ningependa kuchukua pambano hilo,” alisema Thurman. “Nitazungumza na timu yangu na mameneja wangu lakini ninafurahia. Lile lilikuwa pambano zuri. Ningependa kuzichapa na Pacquiao, iwe ni Brooklyn, Las Vegas, sehemu yoyote atakayopenda. Nitapigana naye hata Ufilipino kama atahitaji twende huko,” aliongeza.

Kwa upande mwingine, Kocha wa Manny Pacquiao, Fred Roach alisema kuwa ingawa hakuangalia pambano la Thurman na Lopez, amefurahi kusikia kuwa ameshinda hivyo kama Floyd Mayweather hatakuwa tayari kwa pambano la marudiano, angependa Thurman achukue nafasi.

Majaji wawili wa pambano hilo walimpa ushindi mnono Thurman lakini Jaji mmoja alitoa matokeo ya sare (115-111, 117-109 na 113-113). Lopez (36-8, 19 Kos) alionesha kujitahidi kutorudi nyuma. Ingawa alinaswa na konde moja na kuanguka chini, lakini aliamka na kuendelea.

Thurman alikuwa nje ya ulingo kwa takribani miezi 22, akisumbuliwa na tatizo bega na kiwiko ambapo alifanyiwa upasuaji na sasa asema amerejea akiwa ‘fiti’.

Kakobe awataka Viongozi Chadema watubu au watatumbukia...
Solskjaer ammulika Sanchez, adai yajayo yanafurahisha

Comments

comments