Uongozi wa Klabu ya Yanga umewaomba wanachama wake kuungana kwa pamoja ili kujenga uwanja wao wa mazoezi.

Ombi hilo linakuja kufuatia serikali kutowaruhusu Yanga kutumia Uwanja wa Taifa kufanyia mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Louis ya Shelisheli,

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi, amewaambia waandishi wa habari Jijini Dar es salaam kwamba klabu yao imesikitishwa na kitendo hicho cha serikali kwani inajua kwamba wapo kwenye uwakilishi wa nchi kimataifa.

Mkemi ameeleza kuwa wanachukulia kikwazo hicho kama changamoto kwao na kupata nguvu mpya ya kuendelea na harakati za kujenga uwanja wao wa Kaunda.

Kutokana na hali hiyo, klabu hiyo imeanza rasmi mchakato wa ukarabati wa uwanja wake wa mazoezi ambapo leo katibu mkuu wake, Charles Mkwasa amempokea Mhandisi Christopher Chiza na kumtembeza katika maeneo ya uwanja wa Kaunda ili kupata ushauri wa kitaalum juu ya mradi huo.

Siku ya jana kupitia ukurasa wao wa Facebook, klabu hiyo iliandika ujumbe uliosomeka, “Wakati tukijindaa na mchezo wa kesho kutwa Jumamosi, Yanga imezuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa leo asubuhi na kulazimika kufanya uwanja wa Polisi”.

Taarifa hiyo ya Yanga pia ilimnukuu Meneja wa Uwanja huo, Nsajigwa Gordon akiwaeleza “Huu siyo uwanja wa mazoezi ni uwanja kwa ajili ya mechi, lakini kwa kuwa mgeni hajawahi kuutumia kanuni zinasema ni lazima wapate muda wa kufanya mazoezi kabla ya muda wa mechi,”.

Klabu Kongwe za Yanga na Simba, licha ya kudumu kwenye medani, bado hazina viwanja vyao vya mechi wala mazoezi kama ilivyo kwa Timu ya Azam FC inayomiliki uwanja wake wenye hadhi ya kuchezewa mechi za CAF na FIFA.

Dkt. Mashinji: Baada ya kuona figisu figisu, tumeamua kumuagia kwake
Totenham Hotspurs yaishushia kipigo Arsenal

Comments

comments