Gwiji wa klabu ya Arsenal, Thierry Henry ataendelea kufanya shughuli za ukufunzi wa soka, licha ya kuonyeshwa mlango wa kutokea huko kaskazini mwa jijini London, baada ya kushindwana na bosi wake Arsene Wenger.

Henry ataonekana tena katika tasnia ya ukufunzi, baada ya kuthibitisha kupokea ofa kutoka kwenye klabu mbili tofauti ambazo zinashiriki ligi kuu ya soka nchini England.

West Ham Utd na Watford zinatajwa kumuwania Henry kwa kutojali kazi yake ya uchambuzi wa soka anayoendelea kuifanya kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports, ambacho kilimuajiri mwaka 2015.

Sifa ya kuwa na leseni ya ukocha inayotambuliwa na shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA Pro licence) ndio kichocheo kikubwa kwa klabu hizo mbili kuanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kumpa ajira ya kuwanoa vijana chini ya umri wa miaka 18.

Usiku wa kuamkia hii leo, Henry alithibitisha rasmi kuachana na Arsenal kama kocha wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 18, baada ya kuandikwa kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Aliandika : “Ninapenda kumshukuru sana Andries Jonker, kwa kunipa nafasi ya kuwa kocha wa timu ya vijana ya Arsenal, na bila ajizi nilikubali.

“Hata hivyo, Ninaheshimu maamuzi yaliyochukuliwa na Arsène Wenger dhidi yangu, sina budi kumtakia kila la kheri Kwame Ampadu aliepewa jukumu wa kuwaongoza vijana kwa ajili ya msimu ujao.”

Henry alifanya maamuzi ya kuikacha kazi ya Arsenal, baada ya kushindwa kufuata masharti ya bosi wake (Arsene Wenger) ya kumtaka ajishughulishe na kazi ya ukocha na kuachana na masuala la uchambuzi wa soka katika kituo cha Sky Sports.

Katika kazi hiyo ya uchambuzi, Henry aliwahi kupingana na harakatii za Arsenal kutwaa ubingwa msimu uliopita kwa kumtegemea mshambuliaji wao wa sasa Olivier Giroud, jambo ambalo lilikua kama tusi kwa Arsene Wenger.

Wimbo Mpya: Roma ft Jos Mtambo & Darassa - Kaa Tayari
Waziri Mkuu Akabidhiwa Maabara ya Wananchi waishio vijijini