Baada ya kufanikiwa kutinga Fainali za Kombe la Mapinduzi, Azam FC imetangaza rasmi kumuajiri kocha mpya wa timu hiyo, raia wa Romania, Aristica Cioaba.

Msemaji wa klabu hiyo, Idd Maganga amesema kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa kwa CV ya kocha huyo ndiye anayestahili kuchukua mikoba ya Zeben Hernandez.

Amesema kuwa Kocha huyo ataanza kazi punde baada ya timu hiyo kukamilisha mnyukano wa fainali ya Kombe la Mapinduzi Jumamosi hii.

“Ni kocha mzuri ambaye ameonyesha kwamba anaweza kutusaidia Azam kutokana na CV yake, ndiyo maana uongozi umeamua kumpa nafasi ya kuwa kocha wetu,” Maganga anakaririwa.

Mkufunzi huyo anayetoka kuipika klabu ya Aduana Stars iliyomaliza katika nafasi ya pili ya Ligi ya Ghana atasaini mkataba wa miezi sita kwanza na baadae anaweza kusaini mkataba wa muda mrefu kutokana na makubaliano kati ya pande hizo mbili.

Cioaba ataanza na kazi ya kuking’oa kisiki kizito cha kuhakikisha timu hiyo inaongoza Ligi ya Vodacom Bara ambayo sasa timu yake iko katika nafasi ya tatu kwa pointi 28, ikiwa inazisoma pointi 13 nyuma ya Simba inayoiongoza Ligi hiyo.

Ujio wa Cioba Azam umezima rasmi cheche za tetesi za timu hiyo kutaka kumpa ajira Hans van der Pluijm, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa benchi la ufundi la Yanga baada ya nafasi yake kuchukuliwa na kocha George Lwandamina.

Stan Bakora: Huu ni mwaka wa ubunifu kwa wasanii
Chadema waeleza watakachofanya baada ya mbunge wake kufungwa jela