Baada ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) kutangaza kusitisha msaada wake wa takribani shilingi trilioni moja kwa Tanzania kutokana na kutoridhishwa na ufutwaji wa matokeo ya Zanzibar pamoja na matumizi ya sheria ya mtandao wakati wa uchaguzi, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametuma ujumbe wake kwa rais John Magufuli.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, Mbowe ameeleza kuwa CCM na serikali ya awamu ya nne walitumia ubabe kwa kutumia sheria ya makosa ya mtandao kuwakamata vijana wa Chadema waliokuwa wanajumuisha matokeo kisha kuwabambikia kesi za ‘kugushi’.

Aliongeza kuwa sheria hiyo ya Makosa ya mtandao ilitungwa kwa lengo la kuwasaidia CCM kushinda uchaguzi mkuu kwa kuvibana vyama vya upinzani kwa njia ya mtandao.

“Tuliipinga sheria hii Bungeni na ikapitishwa usiku wa manane kwa ubabe wa wabunge wa CCM na hata tulipomtaka rais Kikwete asiisaini aliisaini kibabe akijua anaandaa mazingira gani ya “kihalifu,” alisema Mbowe.

Kutokana na hayo, Mbowe alimuomba rais Magufuli kushughulikia mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kusaidia mshindi wa uchaguzi huo kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Pia, kuamuru DPP kufuta kesi alizodai zimebambikizwa kwa mgogo wa sheria ya makosa ya jinai na kuwakamata wafanyakazi wa kituo cha haki za binamu (LHRC).

“Kwanza aumalize    mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa mshindi halali anatangazwa. Pili achukue hatua ya kuifanyia marekebisho makubwa Sheria ya makosa ya mtandao katika bunge lijalo. Aidha wale wote waliobambikiwa kesi amuamuru DPP kuzifuta kesi hizo mara moja,” amesema.

Mjumbe Wa Kamati Ya Utendaji Yanga Afunika Kombe
Marekani Yainyima Tanzania Mabilioni kutokana na Kufutwa Matokeo Ya Zanzibar, Ukamataji Makosa ya Mtandao