Kufuatia hatua ya Idara ya Uhamiaji nchini kutaka kumhoji Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhusu uraia wake, baba yake mzazi amejitokeza na kuelezea asili ya ukoo wao.

Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anakabiliwa na kesi mahakamani baada ya kudaiwa kufanya udanganyifu kuhusu tukio lake la ‘kutekwa’, Machi 6 hadi 7 mwaka huu.

Uchunguzi wa jeshi la polisi ulidai kuwa mwanafunzi huyo alipanda basi kutoka Dar es Salaam hadi Mufindi mkoani Iringa na kisha kutuma ujumbe kwa lengo la kuzua taharuki akidai ‘yuko hatarini’.

Akizungumzia asili yake, baba yake Nondo ameiambia ‘Mwananchi’ kuwa baba yake (Babu yake Nondo, mzee Omary Kagobe) alizaliwa mwaka 1919 huko Ujiji Kigoma na kwamba ni mmoja kati ya waasisi wa chama cha TANU.

Alisema kuanzia mwaka 1940 hadi mwaka 1958, babu yake Nondo alikuwa askari wa jeshi la polisi na aliwahi kufanya kazi katika eneo la Mabatini jijini Mwanza.

Aidha, alieleza kuwa mwaka 1970, babu yake Nondo alienda Kuhiji na alipewa hati ya kusafiria ya Tanzania, hati ambayo asingeweza kuipata endapo angekuwa sio raia wa Tanzania.

“Nawashangaa hao wanaomkamata na kumhoji mtoto wangu kuwa sio raia, wananichekesha sana kwa sababu najua mwisho wa siku watajua ukweli,” alisema Mzee.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Nondo aliitwa na kuhojiwa katika ofisi za idara ya uhamiaji na alitakiwa kuwasilisha taarifa za uraia wake ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa vya babu na bibi wa pande zote mbili.

Taarifa hizo zinapaswa kuwasilishwa ifikapo Aprili 20 mwaka huu, kwa mujibu wa Ofisa wa (THRDC), Leopard Mosha aliyedai kuwa alimsindikiza Nondo katika ofisi hizo mwezi uliopita.

 

Profesa Jay akumbuka msoto na jinsi alivyomshangaza Majani
Gereza maarufu la wafungwa wa kisiasa, waandishi lafungwa