Baba wa Marehemu Agnes Gerald, maarufu kama Masogange, Mzee Gerald Waya amesema kuwa baada ya miaka 12 bila kuonana na mwanaye, ahadi ya mwisho aliyompa ni kumtembelea hivi karibuni.

Mzee Waya amesema kuwa mwanaye alimpigia simu mara kadhaa ndani ya mwaka huu, na kwamba simu ambayo walizungumza mengi ni ya Aprili 15 kabla ya simu ya mwisho ambayo ilikuwa saa chache kabla ya kufikwa na umauti.

“Nimekaa miaka 12 nikisali na kutumaini kuwa siku moja nitaonana tena na mwanangu uso kwa uso. Bahati mbaya sasa atarudi nyumbani akiwa ndani ya jeneza,” alisema Mzee Waya.

Akisimulia chanzo cha kutoonana na mwanaye kwa muda mrefu kiasi hicho, alisema walitofautiana baada ya mwanaye kuacha shule akiwa kidato cha pili na baadaye kuhamia jijini Dar es Salaam. Lakini walimaliza tofauti zao na kuanza kuwasiliana kwa njia ya simu wakiamini wataonana tena uso kwa macho.

Aidha, amesema kuwa kutokana na kuikosa nafasi ya kuwa karibu na mwanaye kwa muda mrefu, atamzika pembeni ya nyumba yake ili kuhakikisha wanakuwa karibu kwa kipindi chote ingawa sasa hatakuwa na uwezo wa kuzungumza naye.

Agnes alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu kiasi na kulazwa katika hospitali ya Mama Ngoma iliyoko Mwenge jijini Dar es Salaam. Atazikwa leo nyumbani kwao wilayani Mbalizi mkoani Mbeya.

Kipchoge aibuka kidedea mbio za London Marathon
Wauawa kwa kupigwa risasi ndani ya Mgahawa

Comments

comments