Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 57, mkoani Manyara Kaskazini mwa Tanzania anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania kwa tuhuma za kuwabaka watoto wake watatu wa kike alhamisi ya juma lililopita.

Akitoa taarifa jijini Dodoma kwa waandishi wa habari, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Prudence Constantine amesema kuwa baba huyo anadaiwa kuwafanyia tendo hilo la kikatili mabinti zake hao wenye umri wa miaka 15, 17 na 18.

Constantine alisema kuwa wizara imesikitishwa na taarifa za tukio hilo na inapenda kutoa taarifa kuwa tayari mtuhumiwa yupo mikononi mwa polisi kwa taratibu zaidi za kisheria.

Aidha, amesema kuwa watoto wameshapatiwa huduma za kiafya na wanaendelea kupatiwa huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii

Katika Tukio kama hilo Disemba 13, 2021 Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara lilisema linamtafuta mkazi wa Kata ya Magugu wilayani Babati, Frednand Yohana ambaye anatuhumiwa kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Benjamin Kuzaga alisema mkazi huyo wa Magugu alikuwa anambaka mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 11 (jina lake linahifadhiwa) usiku wakati mke wake na watoto wengine wakiwa wamelala.

Katika taarifa za hivi karibuni za Wizara ya Maendeleo ya jamii zinasema kwamba, kwenye jamii kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili kwenye makundi yote ya jamii ikiwemo watoto, hata hivyo alisema kuwa Wizara inawaomba wananchi kuungana kupinga ukatili wa makundi yote kwa ujumla wake na kutoa taarifa mapema kwenye vyombo vya serikali na vyombo vya kijamii vinavyoweza kutoa msaada wa haraka pale tukio linapotokea.

Simba SC yaomba radhi
Wanandoa ambao hawajashiriki tendo la ndoa miaka 18 wakumbukwa na Mungu