Maofisa wa polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wanawashikilia wanandoa Mary Wambui na mumewe Joseph Maina ambao ni wazee wa kanisa kwa madai ya kuiba mali za kanisa zenye thamani ya Sh300,000.

Wawili hao ambao ni washirika wa kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) tawi la Kang’aru walipanga njama ya wizi na kufanikiwa kuiba mali hizo na kuficha nyumbani kwao wakingojea kutafuta soko.

Kwa mujibu wa Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Hillary Mwaniki amesema kwamba wanandoa hao walitekeleza wizi huo usiku wa kuamkia leo Jumatatu.

Wanandoa hao wanadaiwa kuiba viti 64, kompyuta 1 na vipaza sauti 3, mali ambazo zilikutwa zimefichwa nyumbani kwao.

“Inaaminika kuwa wawili hao walishirikiana na mwanamume mwingine ambaye kwa sasa yupo mafichoni walitekeleza wizi huo usiku wa manane baada ya kuvunja mlango wa kanisa. Aidha, tunachunguza kama watatu hao ndio waliibia makanisa mengine mawili katika eneo hilo usiku huohuo,” akasema.

Bw Mwaniki aliarifu kuwa majirani wa washukiwa hao ndio walitoa taarifa polisi na kisha kutiwa mbaroni.

“Tunawashukuru  raia kwani wao ndio waligundua wezi hao na pia wakawasiliana na maafisa wetu wa polisi ambao waliwasili na kupata washukiwa hao tayari walikuwa wametiwa mbaroni na wenyeji. Ushirikiano huo ulizuilia mali hiyo kuuzwa kabla ya ugunduliwe,” akasema.

Bw Mwaniki alisema kuwa washukiwa hao watafikishwa mahakamani  ili wajibu mashtaka ya kuiba mali ya kanisa huku harakati za kumsaka aliyekimbia zikiendelea kufanywa na polisi.

55 kupigiwa kura Fifpro World XI
Video: Marais wa Afrika waliopunguza mishahara yao