Hatimaye Rais wa klabu ya TP Mazembe ya Congo DR Moise Katumbi amekubali mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ajiunge na klabu ya Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Baba mzazi wa Mbwana, mzee Ally Samatta amesema kwamba Katumbi ameridhia Samatta aende klabu anayopenda.

Wiki iliyopita Samatta alisafiri kutoka Tanzania na kurejea TP Mazembe kwa lengo la kumbembeleza Katumbi abadili msimamo wake wa kutaka kumpeleka Ufaransa na badala yake akubali dili la Genk ya Ubelgiji.

Kwa kipindi kirefu Katumbi alikuwa anapinga Samatta kwenda Genk kwa madai kwamba Genk imetaja dau dogo ikilinganishwa na uwezo wa mchezaji.

“Mwanangu nimemuombea sana kwa Mungu ili mambo yake yafanikiwe na sasa nafurahi sana kuona sasa bwana mkubwa(Katumbi) amekubali aende anakotaka,”alisema mzee Ally Samatta.

“Mazungumzo yao yamekamilika leo na kijana wangu atarejea nchini na kisha atajiandaa na safari ya kwenda Ubelgiji kucheza soka la kulipwa.Nimefurahi sana”

“Pia niishukuru sana Serikali kwasababu kuna muwakilishi mmoja wa Serikali alikwenda Congo kumshawishi Katumbi, kitu ambacho ninafikiri kimeweka uzito wa jambo hili”

Hata hivyo alipotafutwa meneja wa Samatta, Jamal Kisongo kutaka kufahamu kwa undani zaidi juu ya mazungumzo yao jinsi yalivyokwenda hadi Katumbi akakubali lakini akajibu kwamba suala hilo atatolea ufafanuzi siku ya Jumatano.

Man Utd Wakanusha Uvumi Kuhusu Van Gaal
Mwesigwa Afungua Kozi Ya Ngazi Ya Juu Kwa Wanawake