Sintofahamu iliyoibuka kuhusu tetesi za Rich Mavoko kuimwaga lebo ya WCB, imemuibua Meneja wa Bosi wa lebo hiyo, Babu Tale akiyaweka wazi ‘kiutuuzima’.

Meneja huyo amedai kuwa kwa mujibu wa mkataba uliopo, Rich Mavoko bado yuko chini ya lebo hiyo lakini kama kuna mengine muda utakapofika yatawekwa wazi.

Kauli ya Babu Tale imekaa kiutu-uzima na huenda ikaongeza harufu ya tetesi hizo; na kama iko hivyo basi huenda kuna mgogoro wa kimkataba!

“Yupo… kwa sababu contract (mkataba) bado inasema yupo basi bado hupo… kwa sheria ya mkataba bado yupo,” Babu Tale aliiambia Bongo5 na kuongeza kuwa ‘muda ukifika’ wataweka wazi kama yupo au hayupo.

Aidha, Babu Tale alionesha kuwa Rich Movoko akiondoka WCB ni kawaida, akitoa mfano wa ng’ombe ambaye anakula majani eneo moja na kuondoka kuelekea eneo lingine anaposhiba.

“Hata ng’ombe hula manyasi sehemu moja na akishiba anasogea sehemu nyingine. Lakini muda bado wa kuzungumza,” alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Mavoko kufuta kwenye Instagram utambulisho wa kuwa chini ya lebo ya WCB, Meneja huyo mkongwe alitoa mfano kuwa hata Diamond amefuta namba ya meneja wake Sallam kwenye utambulisho wa Instagram yake (bio) lakini haimaanishi kama wawili hao wako kwenye mgogoro.

Tetesi za Rich Mavoko kujiweka kando na WCB zilichochewa na vitendo vya kutoonesha kuunga mkono moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii nyimbo wanazotoa wasanii wenzake pamoja na kufuta utambulisho wa kuwa chini ya lebo hiyo.

Ikumbukwe kwamba wakati Mavoko anasaini mkataba wa kuwa chini ya WCB, alikuwa anatajwa kuwa mshindani mkuu wa Diamond wakati huo.

Usinielewe tofauti, Ali Kiba alikuwa bado yuko mapumzikoni!

Kangi Lugola azikalia kooni kampuni zilizochota fedha za mradi wa NIDA
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 26, 2018

Comments

comments