Tanzania inaelekea kuwa soko la kuzalisha vyombo vya usafiri vya moto vinavyotumika kwa wingi nchini kama Bajaji na Pikipiki ili kuongeza soko la ajira na kuanza kutengeneza nchi aliyoiahidi Rais John Magufuli, ‘Tanzania ya Viwanda’.

Hayo yamebainika baada ya Rais Magufuli kukubaliana na Waziri Mkuu wa India, Narendera Modi aliyewasili nchini hivi karibuni kwa ziara maalum iliyolenga katika kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

“Nimemwomba Waziri Mkuu aone uwezekano wa kuchukua kiwanda kimoja au viwili avihamishie Tanzania vianze kuzalisha hizo pikipiki, bajaji, trekta na hayo magari ili Watanzania wapate ajira pia Tanzania iwe moja ya soko, muwekezaji na mtoza ushuru, amesema anakwenda kulishughulikia,” alisema Rais Magufuli, jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa India.

Rais Magufuli aliongeza kuwa Waziri Mkuu wa India ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania na kwamba kwakuwa nchi hiyo inapenda sana dhahabu inayozalishwa nchini, wamekubaliana kufanya biashara ya ‘win to win situation’ itakayozifaidisha kwa kiwango sawa nchi hizo.

Kadhalika, Rais Magufuli alieleza kuwa India imekubali kuisaidia Tanzania fedha kiasi cha shilingi bilioni 382.4 kwa ajili ya uanzishwaji wa mradi wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, pamoja na mkopo wa shilingi bilioni 197.66 kwa ajili ya usambazaji wa maji.

Waziri Mkuu huyo aliambatana na wafanyabiashara wakubwa 50 kutoka nchini kwake ambao walipata fursa ya kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Sudani Kusini Hali si Shwari
Video: Mitaa Yarindima kwa Shangwe Kubwa, Ureno