Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na vipaumbele vingine inazingatia pia mafungu ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika kila Wizara na Taasisi.

Mhagama ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI – NACOPHA, katika Ukumbi wa Waziri Mkuu uliopo Bungeni jijini Dodoma.

Amesema, “hii ni namna ambavyo Serikali imedhamiria kwa dhati kusaidia utekelezaji wa Afya za masuala ya UKIMWI nchini, kwa kuzingatia maeneo muhimu ikiwemo masuala ya lishe bora, dawa za kupunguza makali ya virusi na kuhakikisha mambo mengine yanayochangia ustawi wao kupatikana”,  amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama akizungumza wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) katika Ukumbi wa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma.

Kuhusu Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001, Mhagama amesema kuna kila sababu ya kufanyiwa mapitio na maboresho kwani ni ya muda mrefu na kuona namna gani sekta zote zinaweza kushiriki katika suala hili ili kuweza kuyafikia malengo ya dunia ya kupunguza vifo, maambukizi na unyanyapaa ifikikapo 2030. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa NACOPHA, Mwalimu Leticia Mourice amempongeza  Waziri Jenista kwa uteuzi wake na pia kumshukuru kwa juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI, aidha aligusia kuhusiana na maandalizi ya Mdahalo wa Kitaifa kuhusu uhimilivu wa mwitikio wa jamii katika mwitikio wa Taifa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Mwalimu Leticia Mourice baada ya kumaliza Mazungumzo hayo.

Kuhusu, uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Taifa, unaolenga utekelezaji wa NMSF5 (Mpango Mkakati wa Tano wa Kitaifa wa Kudhibiti UKIMWI) na alisisitizia  umuhimu wa ushirikiano wa kujenga mwitikio wa kijamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI. 

Awali, akizungumza katika mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuipongeza Serikali ya watu wa Marekeni (PEPFAR/USAID) kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha shughuli za mwitikio wa UKIMWI za NACOPHA na wadau wote wanaotekeleza suala la UKIMWI.

Waaswa usafi wa mwili, Mazingira kukabili magonjwa ya mlipuko
Leandre Willy Onana awindwa Msimbazi