Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inatarajiwa kuwasilishwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango.

Katika Bajeti hiyo inayotarajiwa kutoa picha ya Tanzania ya Viwanda aliyoiahidi Rais Magufuli, imetengewa kiasi cha shilingi trilioni 29.539, ambacho kimezidi kiwango kilichotengwa mwaka jana (shilingi trilioni 22.495).

Serikali imepanga kutumia shilingi trilioni 17.719 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 11.82 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Wakati masikio ya Watanzania yakielekezwa mjini Dodoma leo kufahamu mbivu na mbichi, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imeahidi kuwasilisha bajeti yao mbadala kwa kusoma vipande vichache muhimu na kisha kuondoka Bungeni kwani inaaminika Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ndiye atakayeongoza kikao hicho.

Uamuzi huo wa Kambi Rasmi ya Upinzani umewekwa wazi na Naibu msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde.

Wabunge wa Upinzani waliazimia kutoka nje ya Bunge pale Dk. Tulia atakapokuwa anaongoza vikao hivyo kwa lengo la kuonesha kumpinga. Kambi hiyo imewasilisha hoja rasmi kwa ofisi ya Bunge kuonesha kutokuwa na imani na Dk. Tulia, hoja inayoendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Hillary Clinton ajitangazia ushindi, aandika historia Marekani
Manchester United Wapiga Hatua Usajili Wa Eric Bailly