Kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) Bakari Nyundo Shime ametoa kauli nzito dhidi ya watanzania saa chache kabla ya kuondoka nchini jana jioni, kuelekea mjini Rabat-Morocco kwa ajili ya maandalizi ya kikosi chake.

Shime ambaye anajivunia mafanikio ya Serengeti Boys tangu alipoanza kukinoa kikosi hicho, alisema ni wazi anatambaua ana deni kwa watanzania la kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika fainali za Afrika ambazo zitaanza Mei 14 nchini Gabon.

Alisema deni hilo ni kubwa kwake na kwa wachezaji wa Serengeti Boys, lakini ameahidi kulilipa kwa namna yoyote ile, kwa kuhakikisha kikosi chake kinapambana katika fainali hizo na kufikia lengo.

“Najua uzito wa deni lililo mbele yetu, jibu ni moja tu, ambalo ninaweza kukupa kwa sasa, nitahakikisha tunalilipa kwa kusaka mafanikio bila kujali tunakwenda kupambana na nani huko tuendapo. Najua tutakutana na timu za nchi zenye majina makubwa katika soka hapa Afrika, lakini tutahakikisha tunashinda.” Alisema Shime

Kuhusu maandalizi ya kikosi chake katika michezo mitatu ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Burundi mara mbili na Ghana, Shime alisema ilikua ni kipimo kizuri kwa vijana wake, lakini anaamini watakapofika Rabat-Morocco wataendelea kujiandaa zaidi kabla ya kucheza michezo mingine ya kimataifa ya kirafiki.

“Michezo mitatu tuliocheza hapa nyumbani ilikua ni kipimo kizuri, na imetusaidia sisi watu wa benchi la ufundi kutambua ni wapi tunapokwenda kuanzia katika kambi ya Rabat, tutajitahidi kurekebisha makosa yote kwa kuwahusia vijana wasiyarudie tutakapofika Gabon.” Alisema Shime.

Kikosi cha Serengeti Boys kiliondoka nchini jana jioni saa kumi na dakika 45, kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Morocco kupitia Dubai, Falme za Kiarabu (UAE)

Serengeti Boys itakuwa Rabat, Morocco kwa kambi ya takribani mwezi mmoja. Ikiwa huko itacheza michezo ya kirafiki isizopungua miwili dhidi ya wenyeji Morocco na timu nyingine ya jirani za Tunisia au Misri.

Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu itasafiri hadi Cameroon. Ikiwa Cameroon, timu itacheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambapo Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.

Dar24 inawatakia kila la kheri Serengeti Boys katika mapambano ya kuwania ubingwa wa Afrika kadhalika kucheza fainali za Kombe la Dunia mwezi Novemba, mwaka huu zitakazofanyika India. Serengeti Boys inaweza na Mtanzania tunakuomba kuichangia timu hii kwa namna ya 223344 kupitia mitandao yote ya simu.

Video: Bungeni leo Aprili 6, 2017
Video: Mwakyembe kumbana Makonda maswali tisa, Uchaguzi wabunge AELA kaa la moto